Afisa wa Idara ya Uhamiaji mkoa wa Iringa Tunu Ng'ondya akionyesha hati mbali mbali za kusafiria nje ya Tanzania jana wakati alipozungumza na wanahabari kuhusu kujaza fomu ya Maombi ya Pasipoti kwa njia ya Kielektroniki akiwa mahali popote(picha na Francis Godwin)
Ofisa Uhamiaji mkoa wa Iringa Tunu Ng'ondya amepongeza jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli katika kuboresha idara hiyo na kupelekea kuliletea Taifa heshima kubwa katika dunia kwa kuwa na hati ya kusafiria nje ya Tanzania yenye ubora wa kimataifa .
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake kuhusu kujaza fomu ya Maombi ya Pasipoti kwa njia ya Kielektroniki akiwa mahali popote, Ng'ondya alisema kabla ya jitihada za serikali ya awamu ya tano kufanyika pass hiyo ya kusafiria ilikuwa katika hali ya ubora wa chini ila baada ya kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha idara ya uhamiaji hivi sasa kati ya hati bora za kusafiria duniani hati ya Tanzania ni miongoni na hivyo imeweza kuingia katika ubora wa ulimwengu .
Hata hivyo aliwataka wananchi kufika katika ofisi za uhamiaji kukata pass za kusafiri ili kuweza kuchangamkia fursa mbali mbali za kibiashara nje ya Tanzania kwa kwenda kufuata bidhaa na kuja kuuza nchini ama kupeleka bidhaa zinazozalishwa na watanzania kuuza nje ya Tanzania.
Alisema serikali imeweka utaratibu mzuri wa kila mwenye sifa ya kuwa na hati ya kusafiria kuweza kumiliki pasipo usumbufu wowote na kuwa suala la maombi na malipo ya gharama za kupata pass hiyo yanafanyika kwa njia ya mtandao na kuwa ofisi yake haipokei fedha yoyote taslim kutoka kwa mwombaji isipo kuwa mwombaji anapaswa kufika ofisini akiwa na viambatanishi vya vinavyohitaji baada ya kufanya maombi kupitia mtandao .
" Kama kuna mtu ataombwa fedha taslimu na ofisa yeyote atakapofika ofisini kwangu naomba achukue jina la mhusika na kuniletea ili achukuliwe hatua kali za kinidhamu kwani hatupokei fedha yoyote ile "
Alisema hakuna usumbufu wowote wa kupata hati hiyo kwani ndani ya wiki tatu pekee kwa waombaji wa mikoani wanaweza kupata pass zao baada ya kukamilisha taratibu zote na wale wanaohitaji hati ya haraka wanaweza kupewa ndani ya muda mfupi zaidi .
Ng'ondya alisema mwombaji anayehitaji kupata hati hiyo hatua ya kwanza anapaswa kuingia katika tovuti ya Idara ya Uhamiaji www.immigration.go.tz na kisha kwenda katika kitufe cha e-Services.
Wakati hatua ya pili mwombaji atapaswa kuchagua fomu ya maombi ya hati tatu, kuchagua ombi jipya, nne, atatakiwa kutiki kiboksi kukubaliana na maelekezo na tano anaanza kujaza taarifa zake kwa ukamilifu ukifuata maelekezo na mpangilio katika kila kipengele.
Baada ya mwombaji kukamilisha kujaza taarifa zake, atafahamishwa ya kwamba usajili umekamilika na kupatiwa namba ya ombi, ambayo ni muhimu aiandike pembeni na kuihifadhi kwa kumbukumbu za baadae.
Kuwa mwombaji atapewa namba ya kumbukumbu ya malipo na kutakiwa kwenda kulipia malipo ya awali Sh20,000.
Hata hivyo alisema baada ya mwombaji kumaliza hatua hiyo, ukurasa huo, ataingia katika menu ya M-Pesa/Tigopesa (*150*00#/*150*01#).
Amesema baada ya hapo atatakiwa kubonyeza namba 4 (lipa kwa M-Pesa) au kubonyeza namba 4 (kulipia bili)-Tigo na baada ya kuchagua mtandao wa malipo, atatakiwa kuingiza namba ya kampuni 888999 na mwombaji atatakiwa kuingiza kumbukumbu namba (Ingiza Control Number inayoanzia na 99109…….), kisha kiasi (kama ilivyo elekezwa mfano: 20,000), atapata maelezo kuwa unalipa pesa NMB, baada ya hapo ataingiza namba ya siri, atahakiki na kupata ujumbe mfupi wa maneno kutoka M-Pesa/Tigopesa kama muamala umekubalika.
Kuwa baada ya hatua hiyo mwombaji atapata ujumbe kutoka kwenye mfumo namba 15200 kama muamala umekubalika, kisha kurudi katika ombi linaloendelea na mwisho ataingiza namba ya ombi au simu na namba ya risiti na hapo atapakua fomu yake ya maombi na baada ya kuwa amepata fomu atatakiwa kuiwasilisha katika ofisi ya Uhamiaji wilaya ya Mufindi ,Ilula kwa wilaya ya Kilolo ama makao makuu ya mkoa mjini Iringa .
Social Plugin