Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI AIAGIZA UCSAF KUIWEZESHA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO TTCL


Na Paschal Dotto
RAIS Dkt. John Magufuli ameitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutoa kipaumbele katika uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano kwa Kampuni ya Mawasiliano Nchini (TTCL) ili liweze kumiliki idadi kubwa ya minara ya mawasiliano ya simu  na kumudu ushindani wa soko la mawasiliano nchini. 


Akizungumza katika hafla ya upokeaji wa Gawio la Serikali la Tsh Bilioni 2.1 kutoka TTCL, leo Jumanne (Mei 21, 2019), Rais Magufuli alisema  njia pekee ya kuiendeleza TTCL ni kwa Viongozi na Watendaji wa Serikali kuwa na moyo wa uzalendo wa kusimamia rasilamali za umma ikiwamo za shirika hilo. 


Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema TTCL imekuwa ikitumia kiasi cha Tsh Milioni 700-800 kila mwezi kwa ajili ya kukodisha minara ya mawasiliano, wakati Serikali ina mfuko wa mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unaotoa ruzuku kwa makampuni mbalimbali ya mawasiliano kwa ajili ya kujiwekeza katika miundombinu ikiwemo minara ya mawasiliano maeneo mbalimbali nchini. 


“Hili la TTCL kukopa minara katika makampuni mengine halikubaliki,  Serikali ina mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) ambao wanatoa ruzuku kwa makampuni mengine ya simu lazima tulitazame upya, nataka sasa TTCL tuwape mitaji ya kutosha ili kuhakikisha kuwa linaendelea kupanua huduma zake kwa Watanzania wengi zaidi” alisema Rais Magufuli. 


Aidha Rais Magufuli aliitaka Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inaipatia TTCL kiasi cha Tsh Bilioni 30 kilichobaki kati ya Tsh Bilioni 66 ilizotoa katika mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya kupanua mtandao wa huduma zake nchini, kwa kuwa Shirika hilo limeonesha mafanikio makubwa zaidi katika kipindi kifupi tangu serikali ichukue uamuzi wa kununua hisa zake kutoka kampuni ya Airtel mwaka 2016. 


Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema Serikali itandelea kuiwezesha TTCL ili iweze kupanua mtandao wa mawasiliano yake nchini, na kuhakikisha kuwa linatekeleza vyema majukumu yake ikiwemo kusimamia mawasiliano ya Kimkakati nchini kupitia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa kufuatia kupitishwa kwa Sera ya Taifa ya TEHAMA mwaka 2016. 


Kwa upande wake Mkurugenzi  Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba alisema TTCL imeendelea kupiga hatua kubwa zaidi katika utoaji wa huduma ya mawasiliano nchini ambapo katika mwaka 2018/19, shirika hilo limeweza kupata faida ya Tsh Bilioni 8.3 ambapo kiasi cha Tsh Bilioni 2.1 imetoa gawio kwa Serikali. 


“Katika mwaka 2017/18, tulitoa Tsh Bilioni 1.5, lakini kwa mwaka huu tumetoa Tsh Bilioni 2.1 ikiwa ni ongezeko la Tsh Milioni 600, hii imetokana na kuongezeka kwa makusanyo ya mapato yetu kutoka Bilioni 119 mwaka 2017/18 hadi kufikia Bilioni 167 mwaka 2018/19” alisema Kindamba. 


Kwa  mujibu wa Kindamba alisema TTCL pia imeendelea kusimamia majukumu yake ya msingi ya ikiwemo kuimarisha mfumo wa viwango vya huduma kwa mteja, kujenga uwezo wa teknolojia na miundombinu pamoja na kusimamia mkakati wa mawasiliano kupitia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa. 


Kindammba anasema katika kuwajengea uwezo vijana katika kujiajiri, TTCL kwa kushirikiana na Ofisi ysa Waziri Mkuu imeweza kuajiri vijana 50 waliomaliza vyuo vikuu mbalimbali nchini ambao baadae wataweza kuajiriwa na makampuni mbalimbali ya mawasiliano nchini kwa ajili ya kuongeza mtandao wa utoaji wa huduma ya mawasiliano nchini. 


Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Mhandisi Omary Nundu aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa kwani katika kipindi cha miaka mitatu, shirika hilo limeweza kupata mafanikio makubwa kutokana na maono na dhamira ya Rais Dkt. John Magufuli   kwa shirika hilo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com