Rais John Magufuli, amemtumbua Meneja wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco), Mkoa wa Mbeya, kwa kushindwa kufika kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwa ajili ya upanuzi wa Kiwanda cha Saruji cha Mbeya.
Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, kumhamisha mtendaji huyo kwa kushindwa kufika eneo hilo.
Aliagiza meneja huyo ambaye amefanya kazi katika Mkoa huo kwa miaka minne, atolewe arudishwe alikotoka na apangwe mtumishi mwingine atakayeshughulika na masuala ya umeme.
“Yuko wapi huyo Meneja wa Tanesco, angekuwa hapa si angejibu maswali, Waziri Lukuvi mpigie simu Kalemani, ateue Meneja mwingine wa Tanesco Mbeya kuanzia kesho (leo) aje aanze kazi mara moja,” alisema Rais Magufuli.
Alihoji sababu za meneja huyo kulala nyumbani ilihali mameneja wengine wa idara tofauti katika mkoa huo, walikuwa wamefika katika ziara yake hiyo.
“Mpaka meneja wa Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) yupo hapa nikimsimamisha kazi hapa nitakuwa nimefanya kosa? Wangapi wanakubaliana na mimi, safi kabisa, kuanzia leo yeye ‘out’ akajifunze vizuri kutafuta umeme hatufai tena hapa Mbeya,” Rais Magufuli alisema.
Pia Rais Magufuli aliahidi kufanyia kazi changamoto ya kukatika umeme katika kiwanda hicho linalosababisha hasara kwamba serikali italifanyia kazi.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuboresha utendaji kazi wao na endapo wataendelea kuwa wazembe taasisi za umma ziwanyime zabuni za ujenzi.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana jijini Mbeya wakati akiweka jiwe la msingi katika upanuzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (Must) ikiwa ni siku yake ya tisa ya ziara zake mkoani humo.
“Natoa wito tena kwa mara ya pili kwa TBA waanze kujipanga, wasipofanya vizuri hata kama ni chombo cha serikali msiwape kazi,” alisema Rais Magufuli
Alisema TBA ina wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa wakati katika kazi wanazopatiwa ili kuwahisha miradi ya maendeleo.
“Kwanini mlihangaika kutafuta mkandarasi wa kufanya upembuzi yakinifu na kujenga maktaba wakati kuna wataalam wanafunzi ambao wangefanya kazi ya usanifu? Matokeo yake wamemtafuta mkandarasi aliyewachelewesha kwa miaka saba,” alisema Rais Magufuli.
Rais Maguli alihoji sababu ya kuendelea kuikumbatia TBA ambaye amechelewesha mradi huo kwa miaka yote ilihali wizara yenye dhamana ipo.
Alisema ujenzi wa jengo la maktaba katika chuo hicho, ulianza mwaka 2012 lakini haujakamilika kwa muda wa miaka saba.
Rais Magufuli alisema enzi za Hayati Mwalimu Julias Nyerere, chuo hicho kilijengwa kwa miaka minne kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 1986 lakini maktaba hiyo imejengwa kwa miaka saba na bado haijakamilika.
Aidha, aliahidi kusaidia kulipa deni linalodaiwa chuo hicho la Sh. bilioni 2.9 kwa ajili ya kumalizia kazi awamu ya pili na tatu ya ujenzi wa maktaba hiyo.
Alisema mkandarasi ameshalipwa Sh. bilioni 2.5 na bado hajapatiwa Sh. bilioni 2.9 kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo.
“Hizo Sh. bilioni 2.9 mwezi huu wa tano zitakuja zote sasa ole wenu mzichakachue. Tumuone na huyo mkandarasi kama atashindwa kumaliza kazi,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli aliahidi kutoa Sh. bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya chuo hicho ili kuwafanya wanafunzi wasome kwa uhuru.
Mbali na hilo, Rais Magufuli, aliwaagiza watendaji kumfukuza kazi mkandarasi raia wa China anayejenga barabara ya kuingia katika chuo hicho endapo ataendelea kusuasua kukamilisha mradi huo.
“Hela yote ipo, Sh. bilioni 10.4 ipo, tena mumwambie afanye kazi kwa saa 24 na huu mradi nitaufuatilia mimi. Wamezoea hawa watu wanaomba kazi wakipewa wanaanza kusua sua,” Rais Magufuli alisema.
Aidha, alimwagiza Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa, kupeleka ithibati ya mitaala ya kufundishia fani walizoomba chuo hicho ndani ya siku 10.
Alisema uongozi wa chuo hicho umekuwa ukiomba ithibati kwa muda mrefu bila kupewa hali inayochelewesha kuongeza fani nyingine.
Social Plugin