Rais John Magufuli amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu kutumia muda wao vizuri kujisomea na kuwashukia walimu akiwataka kuwa wakali kwa sababu katika elimu hakuna siasa.
Ametoa kauli hiyo jana Ijumaa Mei 3 mkoani Mbeya katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (Must) baada ya kukasirishwa na tabia ya wanafunzi kutumia muda wao kufanya mambo yasiyo ya msingi hasa kukumbatiana hadharani.
Akiwa katika ziara yake mkoani Mbeya, Magufuli amesema taifa linawekeza fedha nyingi kwa wanafunzi wakati zingeweza kwenda kwa watu wengine kama wakulima, wafugaji, wavuvi lakini imeamua kuziweka katika elimu kwasababu asilimia kubwa inatoka katika familia maskini.
“Mnapokuja hapa vyuoni msidanganyike na makundi, someni wanangu, nilipokuwa nikija hapa nilimuona kijana mmoja amekumbatiana na binti mmoja nikawa najiuliza huyu angekuwa binti yangu ningeteremka hapa ningewazaba vibao wote wawili.”
“Ndiyo ukweli nani atakubali binti yake ambaye amempeleka kusoma atembee njiani ameshikwa na lijamaa ambalo halijatoa hata mahari, lakini ni nani pia mzazi ambaye utamuona kijana wako umemtuma kwenda kusoma kazi yake iwe kukumbatia wasichana.”
“Haya ndiyo matatizo muda mwingine wa vijana wetu, wanashindwa kuelewa walipotoka, walipo na wanakoelekea, Serikali inatumia fedha nyingi kukudhamini kukulipia kila kitu unafikiri huyo akienda darasani atafaulu hapana,” alisema.
Social Plugin