RAIS MAGUFULI ATEMBELEA KIWANDA CHA NYAMA JIJINI WINDHOEK NA ENEO LA MAKABURI YA MASHUJAA WA NAMIBIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 28 Mei, 2019 ametembelea na kuweka shada la maua katika eneo la mashujaa (Heros Acre) waliopigania ukombozi wa Namibia, lililopo nje kidogo ya Jiji la Windhoek nchini humo.


Katika eneo hilo wamezikwa mashujaa wa ukombozi wa Namibia ambao baadhi yao walipata mafunzo katika kambi ya Kongwa nchini Tanzania, wengine walikuwa maafisa wa Chama cha SWAPO ambao ofisi zao zilikuwa Jijini Dar es Salaam na wengine ni viongozi wakuu walioendesha mapambano wakiwa nchini Namibia.

Baadhi ya mashujaa waliozikwa katika eneo hilo ni Ndimo Hamaambo, Peter Nanyemba, Theo-Ben Gurirabo na Toiro ya Toire.

Mhe. Rais Magufuli ameongozana na mwenyeji wake Mhe. Rais Hage Geingob.

Baada ya kutembelea eneo hilo, Mhe. Rais Magufuli ametembelea kiwanda cha nyama cha kampuni Meatco kilichopo Jijini Windhoek na kuelezwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho Bw. Jannie Breytenbach kuwa kiwanda kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 630 kwa siku, kimeajiri wafanyakazi 650 na kwamba kampuni hiyo ipo tayari kushirikiana na Tanzania kuanzisha viwanda vya nyama.

Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania ni nchi ya pili kwa idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika na ameikaribisha kampuni ya Meatco kuja kuwekeza nchini Tanzania.

Katika ziara hiyo, Mhe. Rais Magufuli ameongozana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina, Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi.

Kabla ya kuondoka nchini Namibia kwenda nchini Zimbabwe ambako anakwenda kufanya Ziara Rasmi ya Kitaifa kwa mwaliko wa Rais wa Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Pili wa Namibia Mhe. Hifikepunye Pohamba Jijini Windhoek.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Windhoek
28 Mei, 2019


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post