Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Serikali imesema itaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria wamiliki wa Bar kote nchini wanaopiga muziki mkubwa katika bar zilizokaribu na Makazi ya watu na kusababisha kero kwa Wakazi husika na kukosa usingizi.
Rai hiyo imetolewa leo Mei 22,2019 na Waziri wa Ofisi ya Rais[TAMISIMI]Mhe Seleman Jafo wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Maryam Salum Msabaha aliyehoji ,kuna baadhi ya Bar na Club ambazo zimejengwa kwenye makazi ya watu ambazo zimekuwa na kero kwa jamii kwa kupiga muziki mkubwa na usiozingatia Maadili ya Kitanzania, je,nini kauli ya Serikali kuhusu Bar na Club ambazo zinakiuka maadili ya jamii na sheria.
Katika majibu yake ,Waziri wa Ofisi ya Rais ,TAMISEMI Mhe.Seleman Jafo amesema serikali inawaelekeza wamiliki wote wa Bar na Club kuzingatia maelekezo ya sheria ya Vileo Na.28 ya Mwaka 1968 kifungu cha 14[1] katika uendeshaji wa shughuli zao ambapo amesema serikali haitasita kuchukua hatua kwa vitendo vyovyote vitakavyobainika kukiuka sheria na kusababisha kero kwa wananchi wengine.
Kutokana na Bar na Club kuwa kero katika makazi ya Watu kwa kupiga muziki mkubwa ,Waziri Jafo amewaagiza viongozi wa Serikali za mitaa wakiwemo wakuu wa wilaya na Mikoa kote nchini kufuatilia jambo hilo .
Naye Mbunge wa Rombo,Joseph Selasini amehoji,Mara nyingi Bar zimekuwa zikijengwa kwa kutozingatia mipango miji na watu wenye Madaraka wakiwemo wabunge wenyewe kwanini Serikali isitoe tamko juu ya Bar zinazojengwa Ovyo ovyo iwe Marufuku na mtu atakayetoa kibali cha ujenzi akamatwe.
Akijibu swali hilo,Waziri Seleman Jafo amesema sheria zipo na kinachotakiwa ni kusimamia sheria husika kwa viongozi wa serikali za mitaa na kufanya ufuatiliaji dhidi ya wamiliki wa Kumbi za starehe wanaokiuka sheria hizo.
MWISHO.