Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUPITIA UPYA MASHAMBA YALIYOFUTWA NA RAIS MAGUFULI


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amesema wizara yake itapitia upya mashamba yote yaliyofutwa na Rais katika wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro.

Lukuvi amesema hayo tarehe 16 Mei 2019 katika kata ya Chanzulu tarafa ya Kimamba Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata hiyo ili kutatua mgogoro wa Ardhi katika wilaya hiyo ikiwa ni jitihada za wizara kumaliza migogoro ya ardhi nchini.

Waziri Lukuvi amesema, katika maeneo mbalimbali yapo mashamba yaliyofutwa na Rais lakini hayajawekewa utaratibu  wa kuyatumia na hivyo kutoa fursa kwa wajanja wachache kujigawia na mengine kuyauza kwa wananchi bila kufuata utaratibu.

Amesema katika kuhakikisha mashamba yote yaliyofutwa na Rais katika wilaya ya Kilosa na kuzua mgogoro baina ya wananchi na wamiliki, Wizara yake imeamua kupeleka timu kutoka wizarani kwa ajili ya kuyafanyia uhakiki mashamba yote yaliyofutwa katika wilaya ya Kilosa.

"Tutayapitia mashamba yote yaliyofutwa na Rais na kujua kilichomo ndani yake na timu ya uhakiki niliyokuja nayo itanilitea mapendekezo ya namna ya kutumia mashamba na mengine watapewa wanaostahili na si kila mtu atapewa", amesema Lukuvi

Mashamba yenye mgogoro na wananchi katika wilaya ya Kilosa ni Noble Agriculture Enterprises, Magereza dhidi ya wananchi wa Mabane, Mbigiri na Mabwegere, Chadulu Estate, Shamba la Swai dhidi ya wananchi wa Ilonga na shamba la Mauzi Estate Malangali.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com