Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Katika kukabiliana na tatizo la utapiamlo jambo ambalo hupelekea udumavu kwa watoto ,kwa kusababishwa na lishe duni,Serikali ina mchakato wa kuajiri wataalam wa lishe wawili kwa kila kijiji hapa nchini hali itakayosaidia kutoa elimu ya lishe kwa kila kaya.
Hayo yamesemwa Mei 7,2019 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya ,Maendeleo ya jamii ,jinsia Wazee na Watoto Mhe.Faustine Ndugulile wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum Zainab Mwamindi aliyehoji mpango mkakati wa serikali wa kuajili wataalam wa lishe katika vijiji.
Akijibu swali hilo,Mhe.Ndugulile alisema wizara ya Afya ,Mandeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya Ofisi ya Rais ,Tawala za mikoa na serikali za mitaa,TAMISEMI zina mchakato wa kuajiri wataalam wa lishe wawili wawili kwa kila kijiji kwa ajili ya kutoa elimu umuhimu wa lishe bora.
Hata hivyo,Mhe.Ndugulile amesema serikali inaendelea kupambana na utapiamlo pamoja na lishe iliyopitiliza ambapo asilimia 10 ya Watanzania wanavitambi.
Vipaumbele vya serikali vinavyolenga kupunguza utapiamlo ifikapo mwaka 2021 ni pamoja na kupunguza viwango vya udumavu chini ya umri wa miaka mitano kutoka asilimia 34% mwaka 2015 hadi 28% ,kudhibiti viwango vya ukondefu kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano ibaki chini ya 5% kama ilivyo sasa,Kupunguza viwango vya watoto wanaozaliwa na uzito pungufu kutoka 7% kwa mwaka 2015 hadi 5%.
Vipaumbele vingine ni kupunguza idadi ya wanawake walio katika umri wa uzazi miaka 15 hadi 49 wenye upungufu wa damu kutoka 44.7% kwa mwaka 2015 hadi kufikia 33%,kupunguza tatizo la upungufu wa vitamin A Kwa watoto wenye umri wa miezi 6 hadi miezi 59 kutoka 33% hadi kufikia 26% na kupunguza uzito uliozidi kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano na kubaki asilimia 5%.
Social Plugin