Serikali imeanza kutekeleza mradi wa kusambaza gesi asilia katika miji ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam ikiwa ni nishati mbadala kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu Mgalu aliyasema hayo bungeni jana wakati akijibu swali la Mbunge wa Kibiti, Ally Ungando (CCM).
Katika swali lake, Ungando alihoji Serikali inamkakati gani wa kupeleka nishati mbadala katika Jimbo lake ikiwa ni pamoja ni aina gani ya nishati itakayotumika badala ya kuni na mkaa.
Mbunge huyo alisema wananchi wanaoishi katika Jimbo la Kibiti hutumia kuni kwa matumizi ya nyumbani, shuleni, gerezani hivyo husababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kukata miti hovyo .
‘Je serikali inamkakati gani wa kupeleka nishati mbadala? Na je ni aina gani ya nishati itakayotumika badala ya kuni na mkaa?” aliuliza Ungando.
Akijibu, Naibu Waziri wa Nishati,Subira Mgalu, alisema Mei 18 mwaka 2018 serikali kupitia Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) ilisaini mkataba wa kampuni ya Mihan Gas kwa ajili ya kusambaza vifaa vya kupikia mitungi ya gesi na majiko kwa watumishi wa umma na wananchi wengine mpango unaolenga kupunguza matumizi ya mkaa na kuni.
Mgalu alisema Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015 imetoa muongozo wa kuboresha maisha ya wananchi kwa matumizi bora ya nishati kupitia teknolojia ya kisasa badala ya kuni na mkaa.
Social Plugin