Serikali imeanza mchakato wa kuanzisha BIma ya mazao ili kuweza kukabiliana na changamoto za ukame, mafuriko, magonjwa na wadudu waharibifu.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo bungeni leo, Mei 17, waziri mwenye dhamana, Japheti Hasunga amelieleza Bunge kuwa mfumo huo utamwezesha mkulima kulipwa fidia pale anapopata hasara pamoja na kupata mkopo katika taasisi za fedha.
Amesema kwa kuanzia wizara imeanza kufanya vikao na wadau mbalimbali ili kufanya maandalizi ya awali kwa kuanza na maeneo machache.
“Maandalizi hayo yanaendelea kufanyika ili katika mwaka wa fedha 2019/2020 tuwe anglau na aina mbili za mifumo ya Bima ya mazao inayoweza kutumika nchini” alisema Waziri Hasunga.
Hata hivyo Hasunga alisema ili utaratibu huo uweze kufanikiwa kutahitajika takwimu sahihi za hali ya hewa pamoja na uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo.