Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Serikali imedhamiria kuondoa kero kwa wachimbaji wadogo wa Madini hapa nchini ikiwa ni pamoja na kero za kuondolewa na wachimbaji wakubwa kwani asilimia kubwa wachimbaji wadogo ndio wagunduzi wa kwanza kwenye maeneo ya Madini.
Hayo yamesemwa leo Mei 21,2019 bungeni jijini Dodoma na Naibu waziri wa Madini Stanslaus Nyongo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Rhoda Kunchela aliyehoji serikali iko tayari kutatua kero za wachimbaji wadogo na vibarua ambao wananyanyasika nchini.
Katika Majibu yake Naibu Waziri Stanslaus Nyongo amesema viongozi wanaonyanyasa wenzao serikali ipo tayari kuwafutia leseni zao huku akisema kuwa serikali imekuwa ikiendelea kutatua migogoro ya Wachimbaji wakubwa na wadogo wanaovamia kwenye maeneo yasiyo ya kwao.
Aidha ,Mhe.Nyongo amefafanua kuwa hata mchimba kokoto ana wajibu wa kulipia kitambulisho cha Wajasiliamali wadogo ambacho kilitolewa na Rais John Pombe Magufuli kwa ajili ya Maendeleo ya nchi.
Waziri mwenye dhamana ya Madini, Mhe.Dotto Biteko ametoa wito kwa watozaji wa kodi za madini zilizoondolewa Bungeni waache Mara moja kwani imebainika kuna baadhi ya maeneo hapa nchini wanaendelea kutoza.
Migodi yote nchini inaendeshwa kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 na kuzingatia kanuni za uchimbaji,usalama,mazingira na Afya kwa wakazi.