Ndugu Wanahabari:
Mtakumbuka kuwa 9 Aprili 2019 Serikali ilitoa Tamko la kusitisha matumizi ya Mifuko ya plastiki hapa nchini ifikapo Juni Mosi 2019. Katazo hili linalenga kuepusha athari za kiafya na mazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na matumizi ya mifuko hiyo.
Katazo hilo lililotolewa na Waziri Mkuu Mhe. Kasssim Majaliwa linahusu kupiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usafirishaji nje ya nchi, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko ya plastiki ya aina zote.
Ndugu Wanahabari:
Ofisi ya Makamu wa Rais imekuwa ikitoa taarifa mbalimbali ili kuwaelimisha wananchi kuhusu katazo hilo kupitia Vyombo vya Habari ikiwa ni pamoja na magazeti, Runinga na Redio, Mitandao ya Kijamii, Mikutano ya wadau na kupitia mikusanyiko ya watu ikiwa ni pamoja na taarifa kusomwa katika nyumba za ibaada.
Mpaka sasa Serikali imetekeleza yafuatayo:
1. Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Kanuni kuhusu Katazo hili. Kanuni hizi zitaanza kutumika tarehe 1 Juni 2019. Kwa mujibu wa Kanuni hizi, itakuwa ni marufuku kuzalisha, kuingiza nchini, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki iliyotajwa katika Katazo hili. Kiwanda, Kikundi cha Watu au Mtu Binafsi atakayebainika kukiuka matakwa ya Kanuni hizi atakuwa ametenda kosa la jinai na hivyo sheria itachukua mkondo wake.
2. Tumetoa maelekezo Mahsusi kwa Sekretariet za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu utekelezaji wa katazo hii ambapo baadhi yao wameanza kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya uhifadhi wa shehena ya mifuko itakayosalimishwa
3. Kwa kushirikiana na Makampuni ya Simu ya Vodacom, Tigo, Airtel na Halotel tumefanikiwa kutuma ujumbe mfupi kwa njia ya simu kwa watumiaji wa mitandao hiyo ambapo watumiaji milioni 11 wa Tigo, Milioni 15.5 wa Vodacom wameshapata ujumbe huu, hii itakuwa endelevu kila wiki
4. Tumeandaa na kusambaza taarifa kwenye taasisi za dini ili nao watusaidie kufikisha ujumbe huu kwa waumini wao, tunawashukuru sana wameitikia wito vizuri.
5. Tumekutana na wazalishaji wa mifuko mbadala wa plastiki na wamepanga kuongeza kasi zaidi uzalishaji wa bidhaa hii na baadhi wameshaagiza mitambo ya kuzalisha mifuko mbadala.
6. Tunaendelea kutoa matangazo kwa kutumia vipaza sauti katika ngazi ya Kata, Mitaa na Vijiji kila wiki
7. Tumeendelea kutoa elimu kupitia Vyombo vya Habari ikiwa ni pamoja na kufanya Media Tour, kutoa ‘Count down’ kwenye magazeti, kutumia redio za kijamii na redio za mikoani kutoa matangazo juu ya katazo hili. Pia tumetumia mitandao ya kijamii (Tovuti, blogs, facebook, twitter na istagram) bila kusahau katuni ili kuhakikisha ujumbe unafika kote.
8. Tumetengeneza Bronchure, fliers, Banners na stickers na tunahakikisha tunawasambazia watu wote ili wapate uelewa ikiwa ni pamoja na wasafiri katika Vyombo vya usafiri
9. Tunaendelea na utoaji wa Makala maalumu katika magazeti na kutumia redio kurusha matangazo yetu.
Ndugu Wanahabari:
Jitihada zote hizi zinapaswa kuungwa mkono na si kubezwa, pia nitoe rai kwa watanzania wote kutopotosha jambo hili kama ilivyofanywa juzi katika kipande cha video (Clip) iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii. Na kipande hiko ni cha mwaka jana 2018 wakati wa kikao kilichoandaliwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kuzungumza na Wadau wa mifuko.
Ikumbukwe kuwa ifikapo tarehe 1 Juni 2019, Serikali itaendesha operesheni kabambe nchi nzima ya kusaka mifuko hii. Operesheni hii itahusisha Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya, Mamlaka za Serikali za Mitaa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Shirika la Viwango la Taifa (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, pamoja na Mamlaka za Viwanja vya Ndege, Bandari, Forodha, Uhamiaji, na Usafiri wa Nchi Kavu.
Kwa wale ambao watakuwa tayari kusalimisha kwa hiari shehena ya mifuko watakayokuwa nayo, utaratibu utatolewa wa mahali rasmi wanapotakiwa kuisalimisha kwenye maeneo yao.
Kwa taarifa zaidi kuhusu utekelezaji wa katazo hili Wananchi kwa ujumla mnashauriwa kutembelea Ofisi za Kanda za Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zilizopo Dar es Salaam, Mtwara, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Kigoma na Arusha. Aidha, wanaweza pia kuwasiliana na Wakurugenzi wa Halmashauri za Majiji, Manispaa Miji na Wilaya.
Nirudie tena kutoa rai kwa Watanzania wote kuzingatia maelekezo haya ya Serikali pamoja na matakwa ya Kanuni za kupiga marufuku matumizi na biashara ya mifuko ya plastiki nchini kwa mustakabali wa uhifadhi wa mazingira ya nchi yetu.
Asanteni kwa kunisikiliza,
Imetolewa na:
Balozi Joseph E. Sokoine
NAIBU KATIBU MKUU, OFISI YA MAKAMU WA RAIS
11 MEI, 2019
Social Plugin