SERIKALI YATAIFISHA MAGARI SITA YA WAKILI MEDIAN MWALE


Mkurugenzi wa Mashitaka (DDP), Biswago Mganga amesema serikali imetaifisha rasmi mali za Wakili maarufu jijini Arusha, Median Mwale zenye thamani ya Sh bilioni 1.2 kutokana na makosa ya kutakatisha fedha haramu.

Mganga amesema, mali hizo zilizotokana na zao la utakatishaji fedha haramu baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kumtia hatiani na kuamuru mali hizo zitaifishwe na serikali.

Akizungumzia na waandishi wa habari jana mjini Arusha wakati wa makabidhiano kati ya ofisi ya DPP na Hazina, Mganga alitaja mali hizo kuwa ni magari sita ya kifahari yanayoshikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha.

Mali zingine zilizotaifishwa ni nyumba mbili ikiwemo iliyopo Plot Namba 261 Block C Njiro na nyumba nyingine iliyopo Plot Namba 22 iliyopo eneo la Ilikyurei ambayo ilikuwa mali ya Wakili Loomo Ojale na shamba moja la ekari 10 lililopo eneo la Ngaramtoni.

Alisema hatua hiyo imekuja kufuatia Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kutaifisha mali hizo na kwamba Aprili 14,2019 mahakama hiyo ilitoa kibali cha kuzitaifisha rasmi na kuwa mali ya serikali.

“Kwa mujibu wa sheria mali zinapotaifishwa kuwa mali ya serikali zinakuwa chini ya Katibu Mkuu Hazina” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali Hazina, Benezeth Rutta alisema kuwa Mali hizo baada ya kukabidhiwa kutoka kwa DPP zinakuwa chini ya uangalizi wa Wizara ya Fedha na zinapangiwa matumizi kadri serikali itakavyoona inafaa.

“Mali hizi baada ya kukabidhiwa serikalini zitapangiwa matumizi kadri serikali itakavyoona inafaa na kama itaonekana mali hizo hazifai kwa matumizi ya serikali zitauzwa kwa mnada” alisema Rutta.

Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Selemani Nyakulinga amesema mwaka 2011 alipata taarifa kutoka kitengo cha udhibiti wa fedha haramu kuwa kuna watu waligushi na kutaka kuiba fedha dola za Marekani milioni 17.2.

Alisema fedha hizo zilikuwa zinaibwa kutoka mfuko wa Global Fund kwa ajili ya kusaidia kutibu Ukimwi nchini Tanzania zikitoka Hazina ya nchi ya Marekani.

Amesema walibaini kuwa waliohusika na wizi huo ni raia wa Kenya, wakishirikiana na Watanzania akiwemo Wakili Mwale

Alisema baada ya kufuatilia walifanikiwa kuwatia mbaroni wahusika wote na baadae mahakama ilibaini kuwa wahusika walishanunua mali mbalimbali, zilizotokana na zao la utakatishaji wa fedha hizo na mahakama kuridhia na kutaifisha mali hizo kuwa za serikali.

Credit: Habarileo


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post