Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATOA WITO KWA WADAU KUUNGA JITIHADA ZA UJENZI KITUO CHA KUMBUKUMBU ZA BABA WA TAIFA

Na Anitha Jonas – WHUSM
Serikali yatoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kuunga mkono jitihada za ukarabati na ujenzi  kituo cha kitalii Wilayani Kongwa Jijini Dodoma ambacho kitahifadhi kumbukumbu za Baba wa Taifa Hayati Mwl.Julius Nyerere .


Wito  huo umetolewa leo bungeni  jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari  Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Juliana Shonza  alipokuwa akijibu Swali la Msingi la Mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde (CCM) lililokuwa likiuliza ni lini serikali itajenga maktaba yenye kumbukumbu za kazi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambapo kituo hicho kitakuwa sehemu ya utalii na kitajengwa Makao Makuu ya nchini  ya Jijini Dodoma.

“Katika utekelezaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika,Serikali imeteua Wilaya ya Kongwa kuwa Kituo Kikuu cha Kumbukumbu za ukombozi nchini na katika kituo hicho kitakuwa na miundombinu kadhaa ya uhifadhi wa historia za viongozi ambazo zitajengwa ikiwemo kazi adhimu za Baba wa Taifa,”alisema Mhe.Shonza.

Akiendelea kuzungumza wakati akijibu swali hilo la msingi Naibu Waziri huyo alisema Serikali kwa kushirikiana na UNESCO imekarabati Studio za Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) zilizopo Barabara ya Nyerere na kuwa kituo adhimu cha hifadhi rejea ya kazi za Baba wa Taifa.

Pamoja na hayo Mheshimiwa Shonza  akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Dodoma (CCM) Felister Bura lililohoji lini ujenzi wa kituo hicho cha kumbukumbu cha Kongwa utaanza,Mheshimiwa Shonza alisema ujenzi wa kituo hicho umekwishaanza tangu mwaka 2015 ambapo ukarabati wa kituo hicho ulikwisha anza na unaendelea na pia kuna mipango mikubwa katika kituo hicho ikiwemo kujenga miundombinu ya kisasa mfano hoteli za nyota tano na kiwanja cha ndege.

Halikadhilika katika swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Tabora (CCM)Mwanne Mchemba lini serikali itaingiza katika orodha kituo cha Tabora kutambulika rasmi kama kituo cha kumbukumbu za Baba wa Taifa kutokana na historia yake na mambo aliyoyafanya Mkoani hapo,ambapo Mheshimiwa Shonza alimuhakikishia Mbunge huyo kuwa Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa Mikoa Kumi na Tano iliyoteuliwa kupitia Programu ya Urithi wa Ukombozi  wa Bara la Afrika kuwa vituo vya uhifadhi wa historia hiyo.

Pamoja na hayo serikali inaunga mkono juhudi za taasisi mbalimbali zinazofanya uhifadhi wa amali za Urithi wa kumbukumbu za Baba wa Taifa na baadhi ya taasisi hizo ni Maktaba ya Taifa Dar es Salaam,Makumbusho ya Taifa  Dar es Salaam,Makumbusho ya Mwl.Nyerere Butiama,Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Vituo vya Televisheni vya TBC na ITV.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com