KAGERA SUGAR YAENDELEZA UBABE KWA SIMBA, YANGA SC NAO WAGONGWA 1 - 0 MUSOMA

TIMU ya Kager Sugar ya Bukoba imeendeleza ubabe wake wa kihistoria kwa Simba SC baada ya kuichapa 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.

Nahodha Msaidizi na beki wa kushoto wa Simba SC, Mohamed Hussein 'Tshabalala ' alijifunga dakika ya 41 akiwa katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na Paul Ngalyoma kutoka upande wa kulia kuipatia timu yake ya zamani bao pekee la ushindi leo.

Simba SC ilijitahidi kujaribu kusawazisha bao hilo baada ya hapo, lakini Kagera Sugar inayofundishwa na nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mecky Mexime ilikuwa imara kuzuia.

Kwa matokeo hayo, Simba SC inabaki na pointi zake 81 baada ya kucheza mechi 32 ingawa inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi moja zaidi ya watani wake, Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi tatu zaidi.

Kagera Sugar inafikisha pointi 43 baada ya kucheza mechi 35 na kujiinua kutoka nafasi ya 16 hadi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu yenye timu 20. 

Uwanja wa Karume mjini Musoma, bao pekee la Tariq Kiakala dakika ya nane tu limetosha kuipa Biashara United ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga SC ya Dar es Salaam.

Kiakala alifunga kwa urahisi akitumia uzembe wa mabeki wa Yanga kudhani ameotea kufuatia krosi ya Wilfred Nkouluma katika mchezo ambao, Biashara United ilimaliza pungufu baada ya Nahodha wake, David David Kisu kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 90 na ushei kufuatia kugombana na beki Mwinyi Hajji Mngwali.

Kwa ushindi huo, Biashara United inafikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 34 na kujiinua kutoka nafasi ya 16 kutoka ya 18, wakati Yanga SC inabaki nafasi ya pili na pointi zake 80.

Dar es Salaam kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei/Jonas Mkude dk68, Hassan Dilunga/Rashid Juma dk53, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Clatous Chama dk46.

Kagera Sugar; Said Kipao, Mwaita Gereza, David Luhende, Juma Shemvuni, Peter Mwalyanzi, Kassim Hamisi, Ally Ramadhani, Ramadhani Kapera, Paul Ngalyoma/Majjid Khamis dk69 na Evance Ludovic/ Omary Daga dk57.

Musoma kikosi cha Biashara United kilikuwa; Nourdine Balora, Kauswa Bernard/Taro Donald dk71, Wilfred Nkouluma, Tariq Kiakala, Derick Mussa, George Makang’a/Godfrey Malibiche dk85, Innocent Edwin, Lenny Kissu, Mpapi Nassib, Lameck Chamkaga na Juma Mpakala.

Yanga SC; Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Mwinyi Hajji Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Mohammed Issa ‘Banka’/Mrisho Ngassa dk58, Thabani Kamusoko/Haruna Moshi dk70, Heritier Makambo, Amissi Tambwe na Raphaekl Daudi/Deus Kaseke dk58.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post