Mwenyekiti wa Stand United, Dkt. Ellyson Maeja
Uongozi wa klabu ya wapiga Debe wa Stand United maarufu Chama la wana ya mjini Shinyanga, umesema haujaridhishwa na maamuzi ya shirikisho la soka nchini, TFF, la kuishusha daraja klabu hiyo inayolingana alama na timu ya Kagera Sugar ambayo imebakizwa ligi kuu soka ya Tanzania bara, licha ya Stand United kuongoza kwa magoli mengi ya kufunga.
Mwenyekiti wa Stand United Chama la wana Dk. Ellyson Maeja, amesema wameshangazwa na maamuzi ya TFF ya kuishusha daraja Stand United mara baada ya kumalizika kwa ligi kuu soka ya Tanzania bara, kwa vigezo vya magoli ya kufungwa licha ya kuongoza kwa magoli ya kufunga dhidi ya timu ya Kagera Sugar ambayo inalingana alama 44 katika msimamo wa ligi hiyo.
"Kanuni hii iko bias kwa sababu kwanza, Stand imefunga magoli mengi kuliko Kagera Sugar fc, pili Stand imeshinda mechi nyingi kuliko Kagera Sugar fc,tatu Stand kwa michezo ya face 2 face na Kagera Sugar fc , Stand United fc tumemfunga Kagera Sugar fc 3- 0 kwao Kagera na hapa Shinyanga tulitoka 1- 1 na Stand kwa Kagera katika mechi mbili tulizokutana kachukua pointi 4 na Kagera alipata point moja tu".
"Yaani inauma sana kwa Kagera Sugar fc kupewa zawadi ya kuizidi Stand na Stand kushushwa eti tu kwa Sababu Kagera amefungwa magoli machache tu !!!! Je Stand waliofunga magoli mengi?",amehoji Dkt. Maeja.
"Kuna haja ya wabobezi wa Sheria na kanuni za Soka kusaidia mkanganyiko huu kwa sababu tunaona kuwa kuna walakini katika kanuni ufafanuzi wake na ni kipi kitangulie pale timu zinapokuwa zimefungana point?",ameongeza.
Stand United hadi ligi kuu inamalizika imeshinda mechi 12 na kufungwa mechi 18 magoli ya kufunga magoli 38 na kufungwa 50 huku Kagera Sugar ikishinda mechi 10 na kufungwa mechi 14 imefunga magori 33 na kufungwa magoli 43.
Kufuatia hali hiyo ambayo imeleta mijadala mbalimbali kwa mashabiki wa soka na klabu ya Stand United uongozi umepanga kutafuta washauri na wabobezi wa sheria za soka ambapo klabu hiyo itatoa tamko rasmi la kukubali kushuka daraja au kukata rufaa.