Ndugu Waandishi wa Habari,
1. Nilipata heshima ya kuongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa 109 wa Baraza la Mawaziri wa nchi za Afrika, Karibiani, na Pasifiki (ACP) uliofanyika Brussels, Ubelgiji kuanzia tarahe 20 hadi 22 Mei 2019. Mkutano huu, ulifuatiwa na Mkutano wa 44 wa pamoja wa Mawaziri wa nchi za ACP na wenzetu wa Umoja wa Ulaya (EU) ambao ulifanyika mnamo tarehe 23 na 24 Mei 2019.
2. Katika mkutano huu, upande wa Tanzania niliongozana na Watendaji Waandamizi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Mipango, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Pia, Watalaam kutoka Ofisi ya Ubalozi wetu wa Tanzania Brussels, walishiriki mikutano hii.
3. Aidha, katika mikutano yote miwili, majadiliano yetu yalijikita katika maeneo makuu matatu. Mosi, ni kupitia na kutathimini utekelezaji wa makubaliano na mipango mbalimbali tuliyonayo ndani ya nchi za ACP na baina ya nchi za ACP na EU. Pili, kuainisha, kujadili, na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ushirikiano ndani ya nchi za ACP na baina ya nchi za ACP na EU. Tatu, kutoa muongozo juu ya mustakabali wa ushirikiano tunaotarajia uwepo ndani ya nchi za ACP na baina ya nchi za ACP na EU katika kipindi kijacho.
4. Kwa upande wa agenda ya kwanza, tulipitia utekelezaji wa makubaliano ya programu mbalimbali ndani ya nchi za ACP na baina ya nchi za ACP na EU. Programu hizo ni pamoja na zile zinazohusu masuala ya ubia wa kimaendeleo, biashara, masoko, kilimo, elimu, maendeleo ya sekta binafsi, teknolojia, mifumo ya kodi, uhifadhi wa mazingira, hifadhi ya bahari, na masuala mengine yanayofanana na hayo. Kwa ujumla tulikubaliana kuwa programu hizi ni muhimu katika kuchochea kasi ya maendeleo ya nchi zetu na zikaendelea kutekelezwa kwa kasi inayostahili, mgawanyo ulio sawa na kwa kuzingatia mahitaji ya nchi husika.
5. Kwa mfano, katika eneo la kilimo, Tanzania ilitoa hoja ambayo baada ya majadiliano ya kina ilikubalika kuongeza mazao ya korosho, pamba, na kahawa katika orodha ya mazao yaliyopo katika mpango wa mwaka 2019 wa utekelezaji wa programu ya ACP ya kuendeleza mnyororo wa thamani katika mazao ya kilimo. Mpango huu unafadhiliwa na EU na umetengewa kiasi cha Euro milioni 125. Katika zao la korosho, nchi wanachama wa ACP iliisifu na kuipongeza Tanzania kwa uamuzi wa kishujaa uliochukuliwa na Serikali chini ya uongozi thabiti wa Mhe. Rais Magufuli kwa kuzuia mwendelezo wa mdororo wa bei ya korosho na hatua za makusudi zinazoendelea katika kuongeza mnyororo wa thamani wa zao hilo.
6. Katika kuimarisha sekta binafsi, ujumbe wa Tanzania uliuomba Umoja wa Ulaya kupitia mkakati wa kusaidia sekta binafsi (ACP Private Sector Development Strategy), kuangalia uwezekano wa kuja na mfumo rafiki kwa nchi za ACP, na Tanzania ikiwemo, ambao utawezesha sekta binafsi ya nchi hizo kunufaika. Katika mkutadha huo, ujumbe wa Tanzania uliiomba Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank – EIB), inayosimamia mpango huo, kuanza majadiliano na serikali na kukubaliana namna ya kusaidia sekta binafsi katika utoaji wa mikopo nafuu ya maendeleo (development finance) kwa ajili ya kuchochea uzalishaji na 3 kuongeza thamani ya mazao ya kilimo. Umoja wa Ulaya kupitia mpango wake wa kuwezesha ufanikishaji wa utekelezaji miradi ya kibiashara na sekta binafsi imetenga kiasi cha Euro bilioni 1.1 kwa kipindi cha mwaka 2014 hadi 2020.
7. Wakati wa mkutano huu, ujumbe wa Tanzania ulieleza kwa kina hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano katika kujenga uchumi wa viwanda kwa lengo la kufikia uchumi wa kati. Miongoni mwa hatua tulizozieleza ni pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa uzalishaji wa umeme wa mto Rufiji, ununuzi wa ndege na kufufuliwa kwa ATCL, ujenzi wa barabara, kupanuliwa kwa bandari, viwanja vya ndege na miradi mingine. Tulitumia nafasi hiyo kuzihakikishia nchi za ACP na Umoja wa Ulaya juu ya uwepo wa mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara nchini Tanzania na kuwajulisha kuwa Serikali kupitia mwongozo wa BLUEPRINT inatekeleza mikakati ya kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji na biashara. Hatimaye, tuliwaomba wadau wetu wa maendeleo ndani ya ACP na Umoja wa Ulaya kuunga mkono juhudi hizi madhubuti za Serikali na kuhimiza raia wa nchi zao kuja kuwekeza nchini.
8. Katika agenda ya kujadili changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika ushirikiano wetu, tulibainisha na kujadiliana na wenzetu wa Umoja wa Ulaya juu ya changamoto hizo na umuhimu wa kupata ufumbuzi wake. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kasi ndogo ya utekelezaji wa baadhi ya programu za maendeleo, kiwango kidogo cha biashara baina ya nchi za ACP, kuendelea kuibuka kwa vikwazo vipya vya biashara visivyo vya kiforodha kwa bidhaa za ACP katika soko la Ulaya, sintofahamu inayoendelea baina ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya katika kusainiwa na kutekelezwa kwa Mikataba ya Ubia wa Kiuchumi (Economic Partnership Agreements – EPAs), na kuwepo kwa vikwazo kwa baadhi ya nchi wanachamaa wa ACP na kuwepo kwa maamuzi 4 yasiyozingatia misingi ya uhuru wa nchi (sovereignty), usawa (equal partnership), na kuheshimiana. Nchi za ACP, ikiwemo Tanzania, zilisisitiza changamoto hizi zipatiwe ufumbuzi haraka kwa kila upande unaohusika na tulikubaliana kuwa katika ushirikiano wetu ni muhimu kila upande ukaheshimu kanuni za ushirikiano, sheria na tamaduni za nchi husika. Kwenye hili, Tanzania ikiungwa mkono na nchi nyingine za ACP haja na umuhimu wa kuzingatia na kuheshimu matakwa ya Ibara ya 12 ya mkataba wa ubia wa sasa unaojulikana kama Cotonou Partnership Agreement. Ibara hiyo inazuia upande wowote kuchukua uamuzi wenye madhara kwa upande mwingine bila kuingia kwenye mashauriano ya kina na upande huo.
9. Katika majadiliano yetu, juu ya mstakabali wa ubia mpya baina ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya baada ya ubia wa sasa kufikia ukomo wake ifikapo tarehe 29 Februari 2020, tulipokea taarifa ya majadiliano yanayoendelea. Tulisisitiza mambo makuu matatu. Kwanza, mkataba wa ubia mpya uzingatie zaidi kuziinua nchi za ACP kiuchumi, maendeleo, na biashara. Pili, tulisisitiza umuhimu wa mkataba wa ubia mpya kutohusianishwa moja kwa moja na mikataba mingine ambayo majadiliano yake bado yanaendelea baina ya nchi za ACP na Umoja wa Ulaya ikiwemo mkataba wa EPA na mikataba mingine. Tatu, kwa kuzingatia kuwa tunahitahi majadiliano ya kina na yanayozingatia maslahi mapana ya nchi za ACP, ikiwemo Tanzania, tulitoa fursa kwa majadiliano haya kuendelea hata ikibidi kwa muda wa nyongeza ili kuwezesha zoezi hilo muhimu la majadiliano kwa mstakabali wa ushirikiano wetu na EU kwa miaka mingine ijayo kukamilika kwa ufanisi unaostahiki.
10.Katika hatua ya kuimarisha zaidi ushirikiano na nchi mbalimbali katika ngazi ya kitaifa, kikanda, na kimataifa, hususan kwenye masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, tulipata pia fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa nchi 5 zingine zilizoshiriki mkutano huo. Viongozi tulioonana nao na kufanya mazungumzo ni pamoja na kiongozi wa ujumbe wa Ethiopia, Eswatini, Chadi, Zambia, Equatorial Guinea, Commoro, na Namibia. Pia, tulipata nafasi ya kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi ya Romania na Umoja wa Ulaya. Mazungumzo haya kwa ujumla yametupa uelewa wa pamoja baina ya nchi yetu na nchi hizo kwenye agenda mbalimbali za kitaifa, kikanda, na kimataifa na pia kuimarisha zaidi ushirikiano wenye maslahi baina ya Tanzania na nchi hizo.
11.Ndugu Waandishi wa Habari, kwa ujumla ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano huu ulikuwa muhimu na wenye manufaa. Ujumbe wa Tanzania ulitoa mchango mkubwa na kwa hakika hoja nyingi za Tanzania zilikubaliwa na kuwa sehemu ya maamuzi na maazimio ya mkutano. Tutaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maamuzi na maazimio hayo.
Asanteni kwa kunisikiliza. NAIBU WAZIRI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI 28 MEI 2019, DODOMA