NA WAJMW-DODOMA
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezidi kutoa tahadhari ya kuwepo kwa ugonjwa wa homa ya Dengue nchini hususani katika Jiji la Dar Es Salaam na Tanga.
Tahadhari hiyo imetolewa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Kambi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wizara hiyo zilizoko jijini Dodoma.
Prof. kambi amesema hadi kufikia tarehe 6 Mei 2019, kati ya watu waliopimwa, wagonjwa 1237 wamethibitishwa kuwa na virusi au walikwishapata ugonjwa wa Dengue na kati yao 1150 ni kutoka Dar Es Salaam, 86 ni kutoka Tanga na mtu mmoja kutoka Singida.
Aidha, Prof Kambi amesema takwimu za ugonjwa wa Dengue kwa kipindi cha Januari hadi Aprili 2019 zinaonesha mwenendo wa ugonjwa huu kuwa na idadi ya wagonjwa 1237, vifo vya watu wawili na kuongeza kuwa waliofariki walikua na maradhi mengine.
Pamoja na hayo Mganga Mkuu huyo wa Serikali amelipongeza jiji la Dar Es Salaam kwa kuanza kunyunyizia dawa viuadudu (Biolarvicides) kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu ili kupambana na ugonjwa huu.
Vile vile amesema Wizara inaelekeza Mikoa na Halmashauri zote nchini kuendelea kuchukua hatua katika kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kufukia madimbwi ya maji, kunyunyizia dawa ya kuua viluwiluwi, kuondoa vitu vinavyosababisha mazalia ya mbu, kufyeka vichaka, kufunika mashimo ya maji taka kwa mifuniko pamoja kusafisha gata za paa la nyumba na kutoruhusu maji kusimama.
Prof. Kambi amesema Wizara kwa kushirikiana na Mikoa na Halmashauri zote nchini itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kuendelea kuangamiza mazalia ya mbu na viluwiluwi, kuweka mpango wa dharura wa miezi sita kuanzia Mei mpaka Oktoba ili kukabiliana na ugonjwa huu.
Pia amesema Serikali imenunua Vitendanishi vyenye uwezo wa kupima wagonjwa 1870 na vimesambazwa kwenye vituo maalum vya ufuatiliaji wa ugonjwa huu nchini kote.
Mwisho Prof. Kambi amewataka wananchi kuendelea kuchukua hatua za kujikinga kuumwa na mbu kwa kuvaa nguo ndefu, kutumia vyandarua vyenye viuatilifu, kutumia dawa za kufukuza mbu na kuweka nyavu kwenye madirisha na milango ya nyumba za kuishi ili kukabiliana na ugonjwa huu.