Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAHADHARI YA MVUA KUBWA MWISHON MWA WIKI HII

Mamlaka  ya Hali ya Hewa (TMA) imesema mvua kubwa zaidi inatarajiwa kunyesha mwishoni kwa wiki katika maeneo mbalimbali ya nchi na imewataka wananchi kuchukua tahadhari mapema.

Akizungumza na waandishi wa habari  Dar es Salaam jana, Meneja wa Utabiri, Samuel Mbuya alisema mvua hiyo ni mwendelezo wa mvua ya masika  inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali ya nchi baada ya kutonyesha mwezi uliopita kutokana na kuwapo  kimbunga Kenneth ambacho kilibadili hali ya hewa.

Alisema kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari mapema huku wakiendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa   waweze kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza.

“Mwishoni mwa wiki hii tunatarajia kupata mvua kubwa zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi yanayopata mvua za masika, hivyo basi ni muhimu kwa wananchi kuchukua tahadhari mapema,”alisema Mbuya.

Mbuya alisema  juzi kituo cha kupima mvua cha Pemba kilionyesha kiasi cha mvua ni milimita 105.3 wakati jana iliongezeka na kufikia milimita 181.0.

Alisema  kituo cha kupima mvua kilichopo Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), juzi kilipima kiasi cha mvua kuwa milimita 64.4 na jana iliongezeka hadi kufikia milimita 79.0, wakati Zanzibar ilionyesha 127.3.

Alisema kutokana na hali hiyo  mvua itakayonyesha mwishoni mwa wiki  inaweza kufikia kiwango hicho au kuongezeka zaidi hasa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Zanzibar na Pemba.

Alisema Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Mikoa ya Kanda ya Ziwa itaendelea kupata mvua ya masika kama kawaida, hivyo basi wakulima wanapaswa kufuatilia taarifa za hali ya hewa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com