Waziri Mkuchika akimkabidhi zawadi ya saa yenye picha za
wajumbe wa kamati ya uongozi ya TASAF iliyomaliza muda wake Dr. Florens Turuka,wa kwanza kulia ni mwenyekiti mpya Dr. Moses Kusiluka na kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw.Ladislaus Mwamanga.
Waziri Mkuchika akizindua Kamati ya taifa ya Uongozi ya TASAF katika ukumbi wa Ofisi Ndogo ya Mfuko huo jijini Dar es salaam, kulia kwake ni mwenyekiti mpya wa Kamati Dr. Moses Kusiluka akifuatiwa na mwenyekiti aliyemaliza muda wake Dr. Florens Turuka . Kushoto kwa Mhe. Mkuchika ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga.
Waziri Mkuchika (aliyeketi katikati) katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati mpya ya uongozi ya TASAF na menejimenti ya Mfuko huob aada ya kuizindua Kulia kwake ni mwenyekiti mpya wa kamati hiyo Dr. Moses Kusiluka na kushoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga.
Waziri Mkuchika (aliyeketi katikati ) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya TASAF waliomaliza muda wao baada ya kuzindua rasmi kamati Mpya kwenye Ofisi ndogo ya TASAF jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya menejimenti ya TASAF wakimsikiliza Waziri Mkuchika wakati wa uzindizi wa Kamati ya Taifa mpya kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ndogo za Mfuko
huo jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuchika (wa pili kushoto) akizungumza na Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Uongozi ya TASAF, Dr. Moses Kusiluka (kulia )na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake Dr. Florens Turuka) wa kwanza kulia ,na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus Mwamanga (kushoto ) baada ya kuzindua kamati ya taifa ya uongozi ya TASAF jijini Dar es Salaam.
***
NA ESTOM SANGA-DSM
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteini Mstaafu George Huruma Mkuchika (MB) amezindua Kamati yaTaifa ya Uongozi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF na kuagiza kamati hiyo kuendelea kutilia mkazo suala la utendaji kazi kwa kuzingatia misingi ya uadilifu na uwajibikaji.
Akizindua Kamati hiyo kwenye ukumbi wa Ofisi Ndogo ya TASAF jijini Dar es Salaam, Mhe. Mkuchika amesema Mfuko huo umetekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kujenga jina zuri na hivyo ameagiza sifa hiyo iendelezwe kwa maslahi ya taifa.
Amesema majukumu ambayo TASAF imekabidhiwa yanagusa kwa kiwango kikubwa maisha ya wananchi ambao wanakabiliwa na umaskini na hivyo kutaka Kamati hiyo mpya ya Uongozi ya TASAF kushirikiana na watumishi wa Mfuko huo kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
“mnalo jukumu kubwa mlilokabidhiwa na taifa la kusaidia serikali kupambana na adha ya umaskini na kuboresha maisha ya wananchi,jukumu ambalo ni lazima litekelezwe kwa nguvu na ufanisi zaidi”, amesisitiza Mhe. Mkuchika.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa kamati ya taifa ya Uongozi iliyomaliza muda wake Dr. Florens Turuka akizungumza kwenye hafla hiyo amepongeza hatua ya serikali ya kuendelea kuuamini Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kama njia mojawapo ya kuhamasisha wananchi kupambana na umaskini,na kuwapongeza Watumishi wa Mfuko huo kwa kufanyakazi kwa kujituma kwa manufaa ya taifa.
Naye Mwenyekiti Mpya wa Kamati ya taifa ya Uongozi ya TASAF ,Dr. Moses Kusiluka amesema msingi imara uliowekwa na kamati iliyomaliza muda wake utaendelezwa kwa nguvu zaidi ili kukidhi matakwa ya serikali na wananchi wanaotegemea huduma za Mfuko huo unaogusa maisha ya wananchi wengi.
Dr. Kusiluka pia ametumia fursa hiyo kuagiza uongozi wa TASAF na watumishi wake kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili mfuko huo unaohudumia wananchi wanaokabiliwa na kero ya umaskini waendelee kunufaika na huduma za Serikali kupitia Mfuko huo.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii, TASAF ,bw Ladislaus Mwamanga , ameelezea mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa mfuko huo mwaka 2000 hususani katika sekta za elimu, afya, maji, miundobinu , kilimo,mifugo, uchumi na mapambano dhidi ya umaskini kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao amesema umefanikiwa kuhudumia zaidi ya kaya milioni Moja na Laki Moja katika awamu yake ya kwanza ya utekelezaji kwa aslimia 70 ya mitaa/vijiji na shehia nchini kote.