Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Waziri Kindamba amesema mwaka huu wanatoa gawio la Sh2.1 bilioni kwa Serikali kutokana na kukua kwa mapato ukilinganisha na mwaka uliopita.
Ameyasema hayo leo Jumanne ya Mei 21, 2019 katika hafla ya utoaji wa gawio kwa Serikali iliyoenda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya huduma ya video conference.
Kindamba amesema katika mwaka uliopita mapato yalikuwa Sh119 bilioni na mwaka huu imefikia Sh167 bilioni.
Akizungumza na wafanyakazi wa TTCL, Magufuli amesema: “Tangu Shirikia la TTCL lianze kuendeshwa na wabia wetu, halikuwahi kutoa gawio hata la shilingi tano kwa miaka 15 na lilikuwa likipata hasara ya Tsh bil.15 kwa mwaka, lakini tangu tulirudishe kwenye mikono ya serikali, shirika hili sasa limeanza kutengeneza faida kubwa.
“Niseme kwa uwazi, TTCL mmekuwa mkipigwa vita sana, vita zingine sio za uwazi ni vita vya chinichini, hata leo kuja hapa kulikuwa na mbinu za kijanja-kijanja kunizuia nisije kupokea gawio, na zimechezwa kwelikweli, hii inathibitisha kuwa nyinyi mnastahili, lazima tuwasaidie.
“Waziri amesema Mfuko wa Mawasiliano upo chini ya wizara yake, pesa zinachangwa na Watanzania na TTCL ni ya Watanzania, kwa nini inakodi minara ya mashirika mengine na kulipia Sh mil. 700 hadi mil. 800? Kwa nini usitumie pesa hizo kujenga minara ukawapa TTCL moja kwa moja?
“Mashirika mengine yanalipia kodi, lakini TTCL wanalipa kodi na wanalipa gawio, kwa hiyo faida itayakopatikana itakuwa ni ya serikali, hakuna haja ya kuwaacha TTCL wakateseka, huwezi kumuacha mwanao anateseka na chakula unawapa watu wengine, lazima tuisaidie TTCL.
“Naomba niletewe orodha ya viongozi ambao wanatumia laini za TTCL na sio ziwepo tu bila kutumika, huwezi kulipwa mshahara wa Serikali na hutumii mtandao huo, asije akawa anaandika meseji tu halafu anaicha, nataka ziwe zinatumika, sijamaanisha msitumie mitandao mingine. Msajili wa Hazina hakikisha ifikapo mwezi Julai, mashirika yote 253 nchini ambayo yamekuwa hayatoi gawio kwa serikali, yawe yametoa gawio la sivyo yafungwe.
“Taasisi zilizojiunga kutumia TTCL, ofisi yangu ya rais haikutajwa, chama changu CCM hakikutajwa, inaonekana hawa hata kwenye ofisi yangu wamo. Kama wananisikia ninataka ndani ya mwezi mmoja tuanze kutumia simu za TTCL na wizara nyingine,” amesema.