Ni shindano ambalo lilianzisha safari ya nyota wa sinema za Bollywood Priyanka Chopra, ndio maana shndano la mwaka huu la Miss India limewavutia washiriki wengi ambao walitabasamu wakati walipopiga picha za kujitangaza.
Lakini badala ya wao kujivunia ufanisi wao kwa hatua waliyopiga, wamejipata katikati ya mzozo kufuatia picha ambayo wakosoaji wanasema zinaashiria kuwa waandaaji wa shindano hilo wanavutiwa na watu waliyo na ngozi nyeupe.
Picha hiyo iliyochapishwa katika gazeti la Times la India -haikuwa na neno kwasababu ilionesha kundi la wanawake warembo 30 wanaoshiriki shindano la mwaka huu la Miss India.
Lakini wakati watumiaji wa mtandao wa Twitter walipoanza kuisambaza picha hiyo wakiuliza: "Picha hii ina makosa gani?" ndipo ilianza kuwavutia watu.
Baadhi ya watu waliidhihaki picha hiyo wakisema huenda wote ni mtu mmoja
Kadri picha hiyo ilivyosambazwa mitandao ndivyo ilivyoendelea kupata umaarufu hata hivyo wakosoaji walisisitiza kuwa washiriki hawakuwa na makosa lakini walihoji kuwa shindano hilo liliwavutia watu weupe hatua ambayo iliibua gumzo la jinsi wahindi wanavyoshabikia ngozi nyeupe.
Waaandalizi wa shindano hilo hawajatoa tamko lolote kufikia sasa.
Mashindano ya urembo yamekuwa yakiangaziwa sana nchini India tangu miaka ya katikati ya -1990.
Taifa hilo linajivunia warembo kadhaa maarufu walioshinda mataji ya Miss Indias, kama vile Aishwarya Rai, Sushmita Sen na Bi Chopra, ambao walishinda mataji ya kimataifa.Aishwarya Rai muda mfupi baada ya kuvikwa taji la Miss World 1994
Baadhi ya washindi wa shindano hilo pia walijiunga na tasnia ya uigizaji wa filamu za Bollywood ambayo inasadikiwa kuwalipa vizuri zaidi waigizaji wake.
Kwa miaka kadhaa taasisi zinazowapa mafunzo wasichana wanaotaka kujiunga na masuala ya ulimbwende zimebuniwa kote nchini humo.
Lakini waliyonufaika zaidi na mafunzo hayo ni wanawake waliyo na ngozi nyeupe.
Si jambo la kushangaza
Dhana ya uweupe kuhusishwa na urembo nchini India imekuwepo kwa muda mrefu na kumekuwa na madai kuwa mwanamke mweupe ni mzuri kuliko mweuyeusi.
Krimu ya Fair and Lovely -ambayo inaongeza weupe ilipovumbuliwa miaka ya 1970, ilitokea kuwa bidhaa ya urembo iliyonunuliwa kwa wingi nchini India.
Kwa miaka mingi waigizaji maarufu wa sinema za Bollywood wamekuwa wakifanya matangazo ya biashara ya kuidhinisha krimu hiyo.Waandalizi wa mashindano ya urembo wamekosolewa kwa kuwapendelea zaidi washiriki weupe.
Matangazo ya biashara ya krimu kama hizo ziliwaahidi watumiajiwake sio tu ngozi nyeupe, laini na ya kupendeza bali pia ziliangaziwa kama tiketi ya kumfanya mtu kupata kazi nzuri, mpenzi na kuolewa.
Shindano kama hili linawapendelea washiriki weupe mara nyingi hutumiwa kuendeleza dhana hiyo potovu kuhusu maana halisi ya urembo
Miaka ya hivu karibuni kumezinduliwa kampeini zinazopinga dhana kwamba kuwa ni ngozi nyeupe ndio kigezo pekee cha urembo.
Kupitia Hashtag ya #unfairandlovely, katika mtandao wa Twitter, waandalizi wa kampeini hizo waliwahimiza watu kusherehekea ngozi nyeusi.
Lakini juhudi hizo hazijakomesha kuongezeka kwa bidhaa za urembo zinazodaiwa kuwa na uwezo wa kuwafanya watu kuwa weupe.
Wale wanaounga mkono utumiaji wa bidhaa hizo za urembo wanasema kuwa ni uamuzi wa mtu binafsi lakini kimekuwa na ripoti za mamodo weusi kutengwa wanapotoa maombi ya kutaka kupewa nafasi ya kuigiza katika filamu za Bollywood.
Chanzo -BBC