VIJANA wawili wa Kitanzania, Zakaria Sheha Ally na Shamsi Mwalimu Said wamechukua nafasi ya kwanza na ya tatu kwenye fainali za 27 za tuzo ya kimataifa ya kuhifadhi Quran tukufu.
Zakaria Sheha Ally (16) kutoka Tanzania Bara na Shamsi Mwalimu Said (19) kutoka Zanzibar wameibuka na kitita cha dola za Marekani 5,000 na dola 3,000 kila mmoja baada ya kuwashinda wenzao nane waliofanikiwa kuingia fainali hizo ambao walitoka Afrika Kusini, Sudan, Malaysia, Uturuki, Yemen, Kenya, Burundi na Uingereza.
Nafasi ya pili imechukuliwa na kijana Gaffari Mohammed (14) kutoka Uingereza ambaye ameibuka na kitita cha dola za Marekani 4,000. Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Tanzania, mwaka huu yalishirikisha vijana 10 kutoka nchi 10 duniani.
Tuzo hizo zimetolewa leo (Jumapili, Mei 26, 2019) wakati wa kilele cha mashindano ya 27 ya Kimataifa ya Kuhifadhi na Kusoma Qur’an tukufu na utoaji tuzo yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na mamia ya waumini wa Kiislamu waliofurika kushuhudia kilele cha Tuzo ya Kimataifa ya Quran iliyoandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran nchini, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuhifadhisha Quran kunapaswa kuwa msingi imara katika kujenga jamii bora.
“Tuendelee kuhimiza suala la malezi bora ya vijana wetu kwa lengo la kuwafanya wawe raia wema, wakweli, wazalendo na wenye manufaa kwa nchi yao. Quran inatusisitizia sana kuhusu suala la uadilifu. Kwa mfano, katika Quran 9:119, Mwenyezi Mungu Mtukufu anatukumbusha waumini kumuogopa Mungu na kuambatana na wale walio wakweli wa maneno na vitendo,” amesema Waziri Mkuu.
Amewataka wazazi wa Kiislamu wahakikishe wanawasimamia vema watoto wao na kuwahifadhisha Quran badala ya kutoa msukumo pekee kwenye elimu ya kimazingira. “Sote ni mashahidi kwamba vijana wetu wanao uwezo wa kuhifadhi Quran na wakati huohuo wakasoma na kuhitimu fani mbalimbali katika elimu ya mazingira.”
“Tukumbuke kwamba mafanikio ya duniani na akhera hayapatikani kwingine isipokuwa ni kupitia Quran. Hivyo basi, tuwafunze Quran vijana wetu ili waweze kukabiliana na changamoto nyingi zinazoibuka kwenye ulimwengu wa sasa hususan suala zima la mmomonyoko mkubwa wa maadili,” amesisitiza.
Amesema njia mojawapo ya kuwasaidia vijana kukabiliana na hali ya sasa ya dunia ya utandawazi ni kuwasomesha na kuwahifadhisha Quran. “Vijana waliosoma na kuihifadhi Quran ni vigumu kuenenda kinyume na maadili kwani Quran ndiyo njia pekee ya kuwachunga na kuwafanya waonyeke dhidi ya vitendo vinavyokwenda kinyume na uadilifu.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameipongeza Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran nchini kwa kuendelea kuwapatia vijana wa Kitanzania mwongozo na msingi wa maisha yao kupitia Quran kwani kwa kufanya hivyo wanakuwa wanawaongezea vijana hao uelewa sahihi wa dini yao na elimu ya kutosha ya mazingira (yaani circular education).
“Kwa kufanya hivyo, Jumuiya inalipatia Taifa la Tanzania nguvu kazi yenye uadilifu mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yake sambamba na uwezo na kujiamini katika kuisoma na kuihifadhi Quran tukufu,” amesema.
Amewakumbusha viongozi wa taasisi hiyo watenge muda maalum wa mashindano hayo kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa, kanda, kitaifa ndipo wawagawe kwenye makundi mawili makubwa. “Mkitoka hapo washindanishwe kwa bara la Afrika na kisha mashindano ya dunia. Siyo mnamaliza mashindano ya kimataifa halafu unasikia kuna mashindano ya wilaya au mkoa,” amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na hadhira hiyo, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ali alisema tuzo za leo zimethibitisha kuwa kusoma elimu ya mazingira hakuharibu elimu ya dini. “Iwe changamoto kwa Waislamu kwamba msingi wa elimu ya dini hauchafui elimu ya dini, kwani kuna watu hawataki kusoma elimu ya mazingira kwa kisingizio kuwa mtume hakusoma, sasa mtume atasoma kila kitu?” alihoji.
“Mambo ya uchumi, kijamii, sheria na ufundi yalielezwa na Mtume Muhammad (S.A.W) na Quran imeyazungumzia sana. Kusoma elimu ya mazingira ni muhimu kwa sababu zipo pia aya zaidi ya 70 katika Quran tukufu ambazo zinaelezea mambo hayo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhisha Quran Tanzania, Sheikh Othman Ali Kaporo alisema walilazimika kuanzisha taasisi ili kuwafundisha vijana maadili mema kwani miaka ya 80 - 90 ilikuwa shida kumpata kijana mwenye uwezo wa kuhifadhi hata juzuu tatu tu.
“Hivi sasa taasisi yetu ina vijana zaidi ya 1,000 katika sekta tofauti lakini hakuna hata mmoja aliyekutwa katika mambo ya dawa za kulevya, ufisadi au mambo ya hovyo. Quran ni kinga. Quran ndiyo mafanikio, na kwa malengo hayo, ndiyo maana tunafanya mashindano haya,” alisema.
(mwisho)