Wabunge wa Bunge la Afrika wameziomba nchi zinazokabiliwa na tatizo la wakimbizi barani Afrika kutatua vyanzo vinavyochangia wimbi la wakimbizi ambapo sababu kubwa ni vita na migogoro,ukosefu wa ajira kwa vijana,ubaguzi na kutokuwa na usawa wa kijinsia na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Wabunge hao wametoa ushauri huo leo Jumatatu,Mei 13,2019 wakati wa kikao cha tano cha Mkutano wa pili wa Bunge la tano la Afrika kinachoendelea jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Kikao hicho kilijikita zaidi kujadili kauli mbiu ya Umoja wa Afrika mwaka 2019 ambayo ni "Mwaka wa Wakimbizi,Wahamiaji waliorejeshwa kwao na wakimbizi wa ndani Barani Afrika : Mchango wa Bunge la Afrika katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la uhamiaji wa kulazimishwa barani Afrika".
Wabunge hao wamesema ili kumaliza tatizo la watu kukimbia nchi zao barani Afrika, ni vyema serikali zikapiga vita vyanzo vya ukimbizi ikiwemo kuzingatia demokrasia na utawala bora huku viongozi wakiacha tabia ya kung'ang'ania madarakani.
Akichangia hoja bungeni,Mhe. David Silinde kutoka Tanzania alisema watu hawawezi kurudi kwenye nchi yao kama ile amani iliyokuwa imepangwa kuwepo haipo kwa hofu ya kulipiziwa kisasi na hata kupoteza maisha yao wakirudi kwenye maeneo yao.
"Kwa hiyo sisi tunatakiwa tujikite kwenye kuhakikisha kunakuwa na uongozi bora katika nchi zetu,tuondoe siasa mbaya ambayo imekuwepo kwa kipindi kirefu kama watu kung'ang'ania madaraka na tutokomeze vita ya wenyewe kwa wenyewe,kwa kufanya hivyo tutakuwa sasa tumetatua chanzo kikubwa kinachohusu watu wengi kukimbia katika nchi husika",aliongeza Mhe. Silinde.
Alieleza kuwa,kutokana na kwamba dunia inafahamu na Afrika inajua nchi zote ambazo zina matatizo yanayohusika na wakimbizi wengi,ni vyema nchi za Umoja wa Afrika zikashirikiana kulitatua tatizo la wakimbizi kwa kuanza na wao wenyewe na wala siyo kusubiri msaada kutoka Umoja wa Mataifa.
Wakichangia katika mjadala huo uliodumu kwa takribani saa nne. Mhe.Roumba Workya kutoka Burkina Faso na Suilma Hay Emhamed Elkaid kutoka Jamhuri ya Sahara Magharibi (Sahrawi Republic) walisema tatizo la ukimbizi linaumiza hivyo ni vyema serikali za nchi za Afrika zinatakiwa kutatua vyanzo vinavyosababisha watu wakimbie nchi zao huku wakikisitiza kuwa hakuna mtu anayependa kuwa mkimbizi.
Naye Mhe. Mboni Mhita kutoka Tanzania alisema ili kuwa na suluhisho la kudumu la wakimbizi ni vyema kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana,migogoro ya kisiasa na dini huku akiyashauri Mashirika yanayohudumia wakimbizi kusaidia kutatua vyanzo vya ukimbizi.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR),takwimu za mwaka 2017 zinaonesha kuwa duniani kote kuna wakimbizi milioni 23 kati yao Afrika kuna wakimbizi milioni 7 huku masuluhisho ya kudumu yakitajwa kuwa ni wakimbizi kurudi nyumbani kwa hiari,kupewa uraia/makazi ya kudumu katika nchi iliyowapokea,kusaidiwa kupewa makazi mapya ama mkimbizi mwenyewe kwenda nchi ya tatu mfano kujiunga na familia yake,ajira au masomo.
Na Kadama Malunde - Afrika Kusini
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO MBALIMBALI BUNGENI
Wabunge wa bunge la Afrika wakifuatilia mjadala kuhusu kauli mbiu ya Umoja wa Afrika mwaka 2019 ambayo ni "Mwaka wa Wakimbizi,Wahamiaji waliorejeshwa kwao na wakimbizi wa ndani Barani Afrika : Mchango wa Bunge la Afrika katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la uhamiaji wa kulazimishwa barani Afrika". Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog Afrika Kusini.
Mhe. David Silinde kutoka Tanzania akichangia hoja katika bunge la Afrika.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika,Mhe. Stephen Masele akimsikiliza Mhe. David Silinde kwa umakini ukumbini.
Makamu wa Nne wa Rais wa Bunge la Afrika,Mhe. Chief Charumbira akifuatilia mjadala bungeni.
Makamu wa Nne wa Rais wa Bunge la Afrika,Mhe. Chief Charumbira akifuatilia mjadala bungeni.
Mhe. Mboni Mhita akichangia hoja bungeni.
Wabunge wakiwa ukumbini.
Bunge likiendelea.
Wabunge wakiwa bungeni.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Social Plugin