Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inaangalia uwezekano wa watanzania wanaoishi nje ya nchi kuweza kupiga kura katika uchaguzi ujao.
Kauli hiyo ameitoa leo Mei 23 wakati akijibu maswali ya papo kwa papo bungeni ambapo alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Asha Abdalah Juma (CCM).
Katika swali lake Mbunge huyo ametaka kujua serikali ina mpango gani wa kuwashirikisha watanzania wanaoishi nje kupiga kura katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
“Ilani ya Chama cha CCM imetekelezwa kwa kiasi kikubwa pamoja na mambo mazuri je serikali ina mpango gani wa kuwawezesha watanzania wanaoishi nje waweze kupiga kura mwaka 2020” amehoji
Akijibu swali hilo Majaliwa amesema suala hilo ni la kisera na kwa sasa serikali inalifanyia kazi kuona jinsi gani watanzania hao wataweza kupiga kura.
Amesema ni lazima kwanza kujua idadi ya watanzania hao waliopo nje na wanafanya nini
“Hili ni jambo la kisera lakini kwanza tujue idadi yao na wapo wapi na wanafanya nini kabla ya kuruhusu kupiga kura” amesema
Akizungumzia suala la miradi ya maji amesema ipo miradi ambayo imegundulika kuwa chini ya viwango na serikali imeshaanza kuchukua hatua na kuweka wasimamizi toka mikoani hadi ngazi ya halmashauri.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema pamoja na kuwepo kwa miradi mingi ya umwagiliaji lakini bado suala la kilimo cha umwagiliaji hakijatoa tija kwa taifa.
“Tayari tumeshavunja Tume ya umwagiliaji kwa sasa tunaipeleka kwenye wizara ya maji” amesema