Na Amiri kilagalila-Njombe
Waziri wa maji Prof. Makame Mbarawa ameagiza jeshi la polisi kumshikilia kwa saa 24 Mkandarasi wa kampuni ya Water and Earth Works Ltd (BWE ) Emmanuel Mzena anayesimamia mradi wa maji bwawani mjini Makambako mkoani Njombe kutokana na kushindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati.
Waziri Mbarawa alifikia uamuzi huo jana mjini Makambako wakati alipotembelea mradi huo.
“Nataka kesho watu wako waje kwenye site na wewe utakaa ndani leo mpaka kesho kwa masaa 24, kama watu wako hawata kuja tutakuingiza tena hivyo hivyo mpaka utaleta wafanya kazi ujinga sitaki kuusikia, na ninyi makandarasi mpaka muwekwe ndani ndio mfanye kazi,wananchi wote hawa watoto wadogo wanaharisha ninyi mmepewa pesa za serikali hamfanyi kazi mnajifanya mnajua sheria kumbe nyie ndio wezi wa serikali”alisema Mbarawa
Aidha waziri huyo amemtaka mkurugenzi wa mamlaka ya maji mjini makambako kusimamia mradi huo kwa kuhakikisha tanki la maji la mradi huo linajazwa maji na akishindwa naye atawekwa ndani.
Awali akizungumza kuhusiana na mradi huo kushindwa kukamilika kwa wakati na kushindwa kuendelea na kazi katika mradi huo mkandarasi huyo Emmanuel Mzena amesema wameshindwa kuendelea na kazi kutokana na malipo yao kucheleweshwa.
“Ni kwamba tumesimama kwasababu tulifanya kazi lakini tumechelewa kulipwa na certificate ya mwisho tulilipwa mwezi wa 9,lakini mkataba unasema mkandarasi akiwa anaendelea na kazi anaendelea kulipwa”alisema Mzena
Huseni Nyemba ni mkurugenzi wa mamlaka ya maji mjini makambako amesema kuwa kutokana na agizo la waziri tatizo hilo linafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo licha ya kuwa mradi huo unasimamiwa na mamlaka ya maji safi na usafi wa wa mazingira Iringa (ILUWASA).
“Huu mradi ulikuwa kiu yetu lakini wananchi wanatakiwa waelewe mradi ule walioingia mkataba ni mamlaka ya maji mkoa wa Iringa na wenyewe ndio wapo kisheria na kiutaratibu wa kimkataba sisi mamlaka ya maji Makambako ni kama wanufaikaji baada ya mradi kukamilika ,nashkuru leo waziri alipotoa maagizo ni kama ametupatia ufunguo”alisema Mkurugenzi
Mradi wa huo wa maji Bwawani ulianza mwaka 2017 na ulitakiwa kukamilika mwezi wa sita mwaka 2018 lakini mpaka sasa haujakamilika.