Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) leo tarehe 9 Mei, 2019 ameiagiza Timu ya wataalamu wa wizara ya Kilimo ambao wametuama kuandaa rasimu ya sheria ya kilimo na kufikia mwezi Julai 2019 iwe imekamilika.
Alisema kuwa ipo haja ya kuanzishwa kwa Sheria ya Kilimo itakayotoa suluhisho la changamoto zinazomkabili Mkulima na Sekta hiyo kwa ujumla hivyo ili kufikia malengo hayo ni lazima kuwa na ukomo wa ukamilishaji wa mpango kazi huo.
Waziri Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 9 Mei 2019 wakati wa kikao na Menejimenti ya Wizara ya Kilimo, kikao kilichohudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe.
“Kuna kila sababu ya kuanzishwa haraka sheria ya kilimo, kwa sababu hatuna Sheria ya Kilimo na inayotumika sasa ni Sera ya Kilimo, iliyotungwa mwaka 2013 ambayo pia inahitaji kuboreshwa ili iweze kuendana na mabadiliko mbalimbali ya kisera na wakati, ambapo lazima tuwe na rasimu yake kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Mei” amesema
Mhe. Hasunga ameongeza kuwa Sheria zinazotumika kwa sasa ni za Bodi za Mazao mbalimbali, ambazo pia zinachangamoto zake na kuna mazao ambayo hayana Bodi kiasi kwamba kuwatetea Wakulima wa mazao hayo inakuwa vigumu.
Mazao yaliyo katika utaratibu wa Bodi ni pamoja na zao la Pamba, Kahawa, Chai, Korosho, Pareto, Mkonge, Sukari na Tumbaku kwa upande wa mazao ya biashara, mazao ambayo hayana bodi ni yale ya chakula ambayo nayo yana mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Innocent Bashungwa (Mb) alisema kikao hicho ni cha kipekee kwakuwa kitapelekea kuimarisha mkakati wa pamoja wa Wizara ya kilimo kuwa na uelekeo katika utatuzi wa kero za wakulima kisheria.
Aidha, alipendekeza kuwa ni vyema sekta ya ushirika ikatajwa kwa umuhimu wake kwenye sera ya kilimo sambamba na Zana ndogo za Kilimo.
Social Plugin