Waziri Kivuli wa Nishati, John Mnyika, ameitaka serikali iwasilishe bungeni mkataba wa utekelezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa Stiegler's Gorge pamoja na mikataba yote ya bomba la gesi Mtwara na ripoti zote zilizotokana na kamati zilizoundwa kuhusu mafuta na gesi ili Bunge iipitie.
Pia ametaka serikali iwasilishe ripoti ya tathmini ya kimazingira iliyofanyika ya utekelezaji wa mradi wa Stiegler’s ili Bunge lione athari zake.
Mnyika aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa mikataba hiyo pamoja na ripoti hizo ziwasilishwe bungeni kesho wakati waziri akiwasilisha hotuba ya wizara yake.
Akizungumzia kuhusu mkataba wa Stiegler’s, Mnyika ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kibamba (Chadema), alidai umekuwa na mkanganyiko wa gharama zitakazotumika, hivyo ametaka upelekwe bungeni ili waone ni miujiza gani iliyofanyika kutoka utekelezaji wake wa miaka 12 awali hadi miaka mitatu sasa.
“Binafsi nimeshaandaa rasimu ya hotuba yenye kurasa 80 na aya 145 inayozungumzia mambo mbalimbali ya sekta ya umeme, gesi na mafuta,” alisema.
“Serikali ilileta bungeni muswada wa sheria unaohusu sekta inayogusa rasilimali za nchi, muswada mmojawapo ukiwa na kifungu chenye kutoa wajibu na haki kwa Bunge na wajibu kwa serikali kwenye mikataba mikubwa ya nchi inayogusa rasilimali za nchi.
“Mikataba hii ilikuwa na kifungu kwamba inabidi ipelekwe bungeni kwa sababu kumeshatokea utata wa mradi wa Stiegler's Gorge, wito wangu ni kwamba tarehe 28 (Jumanne) wakati waziri anasoma hotuba yake bungeni pamoja na hotuba ya serikali, awasilishe mkataba wa ujenzi wa mradi wa Stiegler's ili mbivu na mbichi zijulikane.”
Mnyika alisema serikali ilisema mkataba ambao umesainiwa na mkandarasi ni wa Sh. trilioni 6, lakini awali iliwahi kusema mradi mzima utagharimu Sh. trilioni 10.
“Uchambuzi mbalimbali ukianzia na wa serikali yenyewe ikiwamo Wizara ya Nishati na Madini wakati huo (mwaka 2016) ilifanya uchambuzi kuhusu gharama za mradi huu ambao ungetumia miaka 12 kujengwa, hii ni kwa tathmini ya wizara na tathmini ya wataalamu kuanzia mwaka 2012,” alisema.
Credit: Nipashe