WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Pekka Hukka na kumshukuru kwa jitihada za nchi hiyo kuisadia Tanzania kuondokana na umaskini.
“Tunaishukuru Serikali ya Finland kwa misaada ambayo imeendelea kuitoa kama njia ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania za kuondoa umaskini pamoja na kuongeza makusanyo ya mapato ili kukuza uchumi wa nchi yetu,” amesema Waziri Mkuu.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Mei 23, 2019) alipokutana na Balozi huyo anayemaliza muda wake wa kazi hapa nchini, ofisini kwake bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amemweleza balozi huyo kwamba Tanzania bado ina fursa za uwekezaji na kwamba Serikali inaendelea kutengeneza mazingira rafiki na bora kwa uwekezaji. “Sekta ambazo makampuni ya Finland yanaweza kuwekeza hapa nchini ni pamoja na TEHAMA, nishati, usafiri, uchakataji wa mazao ya kilimo na misitu,” amesema.
Waziri Mkuu alimtakia heri Balozi Hukka ambaye anatarajiwa kuondoka nchini mwishoni mwa mwezi huu kwenda Tunisia ambako ndiko kutakuwa na kituo chake kipya cha kazi.
Kwa upande wake, Balozi Hukka alisema ataondoka Tanzania akiwa na kumbukumbu nzuri ambazo atazienzi na anataraji kukutana na Watanzania wengine ili aendelee kukuza mahusiano yaliyokuwepo.
Alisema Serikali za Tanzania na Finland zilisaini mkataba wa programu iitwayo Forestry and Value Chain Programme (FORVAC) ambao unalenga kuongeza faida za kiuchumi na kijamii kwa kupitia sekta ya misitu pamoja na kupunguza ukataji wa miti. “Malengo hayo yatafikiwa kwa kukuza mnyororo wa thamani kwenye sekta ya misitu pamoja na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, sheria na sera katika sekta ya misitu,” alisema.
Finland inasaidia sekta ya misitu nchini Tanzania kupitia Programu ya Private Forestry Programme (PFP) ambayo ililenga kuongeza mapato kwa wakazi wa vijijini katika Halmashauri 10 za Njombe TC, Njombe DC, Makete, Ludewa, Kilombero, Mufindi, Kilolo, Madaba, Mbinga na Nyasa) kwa kusaidia upandaji wa miti na kuongeza thamani ya mazao ya misitu.
Programu hiyo imesaidia kujenga uwezo kwa wahusika wote katika mnyororo wa thamani wa biashara ya mazao ya misitu. Awamu ya kwanza ya programu hiyo imesaidia kuongeza kipato cha familia zaidi ya 9,000 kwenye wilaya hizo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekutana na Balozi wa Uswisi hapa nchini, Mhe. Florence Mattli ambaye pia alienda kumuaga ofisini kwake bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mkuu alimweleza balozi huyo dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kudumisha ushirikiano na Uswisi na kusisitiza kwamba iko tayari kufanya kazi na Balozi mpya wa Uswisi atakayekuja kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Ni muhimu sana ushirikiano wa Tanzania na Uswisi ukadumishwa kwa kuzingatia pia masuala ya biashara na uwekezaji hususan kwenye sekta za afya, kilimo, elimu na teknolojia,” alisema Waziri Mkuu.
Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Uswisi kwa misaada ambayo imeendelea kutolewa na nchi hiyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania za kuondoa umaskini hususan kwenye miradi ya afya, kilimo na uwekezaji katika elimu na biashara kwa ajili ya kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Balozi Mattli alisema Serikali ya Uswisi imekuwa ikiunga mkono na kusaidia jitihada za kukuza uwazi na uwajibikaji kwa watendaji wa Serikali na wale wasiokuwa wa Serikali kuzingatia mazingira ya kitaasisi na kijamii yanayopiga vita masuala ya rushwa.
“Msaada huo wa kupambana na rushwa umechangia kuimarisha ufanisi wa uendeshaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kukuza uelewa wa kijamii kuhusu masuala ya rushwa,” alisema.
Alisema mwaka 2018, Serikali ya Uswisi ilitoa dola za Marekani milioni 24 kusaidia Mpango wa Ukuzaji Ujuzi kwa Ajira Tanzania, ambao ulianza kutekelezwa Agosti Mosi, 2018 kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
“Mpango huo unalenga kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa vitendo na kuimarisha mafunzo ya ufundi nchini. Hivyo, mpango huo umechangia kuboresha matarajio ya vijana kwa kuwapatia ujuzi katika kazi na ubunifu unaochangia kuondokana na suala la ukosefu wa ajira,” alisema.
Alisema Serikali ya Uswisi inasaidia maendeleo ya vijana kupitia Mpango wa Ajira ya Vijana (OYE) ambao unalenga kuimarisha maisha ya vijana wa kiume na wa kike kwa kuwafundisha fursa za ajira katika sekta za biashara, kilimo, nishati mbadala, usafi wa mazingira na kuboresha ujuzi.