Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Luhaga Mpina amesema serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria watu wanaofanya ukatili kwa wanyama ambapo amesema ifikapo tarehe 1.Julai ,2019 watendaji wanaoshikilia mifugo hadi kufa ikiwa mikononi mwao watashughulikiwa.
Mhe.Mpina amesema hayo leo Mei 22,2019 Bungeni jijini Dodoma ambapo amesema mifugo ni rasilimali za nchi kama rasilimali nyingine na wizara yake haitavumilia kuona mtendaji wa Serikali akishikilia mifugo mpaka ina kufa kwa kigezo cha kufuata sheria kwani hata mifugo nayo ina sheria zake.
Awali ,Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Abdallah Ulega wakati akijibu swali la mbunge wa Wa Morogoro Kusini Prosper Mbena aliyehoji juu ya ukatili wa wanyama kushamiri nchini ,chama cha kuzuia ukatili wa wanyama Tanzania ,TSPCA kina shirikiana kwa kiasi gani na Serikali ili kuzuia ukatili ,Mhe.Ulega amezitaja sheria za wanyama pindi wanapokamatwa ikiwa ni pamoja na kupatiwa malisho,maji na chanjo.
Kuhusu uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata na kusindika nyama katika maeneo yaliyo karibu na wafugaji ili kupunguza ukatili wa wanyama pindi wanaporundikwa kwenye magari wakati wanaposafirishwa Kwenda Dar Es Salaam kwa ajili ya kuchinjwa,Mbunge wa Msalala Ezekiel Maige amehoji lini serikali itaanzisha viwanda katika maeneo mbalimbali ya wafugaji nchini ikiwa ni pamoja na Shinyanga.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema mchakato wa kufufua viwanda vya kuchakata na kusindika nyama nchini upo palepale na kinachotakiwa ni kupata mwekezaji aliyejipanga vizuri.
Hata hivyo,Serikali inashirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kama TSPCA katika kudhibiti vitendo vya kikatili kwa wanyama kwa kuzingatia sera ya mifugo ya mwaka 2006 na sheria ya Ustawi wa wanyama ya mwaka 2008 kwa kuelimisha jamii.
Mwaka 2018 jumla ya Makosa 3,542 kwa kosa la ukatili wa wanyama yaliripotiwa ambapo ni ng’ombe 847 ,mbuzi na kondoo 1,578,nguruwe 88,kuku 539 na punda 490. .