Na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amelishauri Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF), kuweka namna bora ya kuingiza ajenda ya uwekezaji kwa watoto katika mikutano mbalimbali inayofanyika Barani Afrika.
Hayo ameyasema alipokuwa akiagana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) Bi. Maniza Zaman, anayehamia nchini Kenya.
Dkt. Mpango alisema Shirika hilo linatakiwa kuweka mkazo huo ili kuhakikisha nchi za Afrika zinaweka mipango ya kuwekeza kwa ajili ya watoto kwa kuwa kundi hilo ndiyo Taifa la kesho.
Alisema Serikali ya Tanzania kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Elimu Nchini, imekuwa ikitoa kipaumbele katika elimu kwa kutoa elimu ya awali, msingi na sekondari bure kwa lengo la kutoa nafasi kubwa kwa watoto ili wapate haki yao ya msingi.
Aidha Dkt. Mpango alisema kuwa katika kuboresha Sekta ya Elimu Duniani ni vema pia masuala ya lishe bora kwa mtoto yakatiliwa mkazo kwani lishe bora inachangia afanye vizuri dararasani lakini pia itamsaidia mtoto kuwa na afya bora itakayomfanya aweze kufikiri vizuri.
“Nitahakikisha agenda za kulinda haki ya mtoto nchini inapewa kipaumbele kwenye mikutano yetu mikubwa tunapokuwa tukijadili masuala ya maendeleo kwa ujumla”, alisisitiza Dkt. Mpango.
Aliongeza kuwa jukumu la kumlinda mtoto ni la kila mmoja kwakuwa wote walishawahi kuwa watoto hivyo ni vema kila mmoja atomize jukumu hilo.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) Tanzania Bi. Maniza Zaman, anaye hamia nchini Kenya, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kufanya nae kazi vizuri kwa kipindi chote alichokaa nchini.
“Tanzania ni nchi nzuri, watu wake wana upendo, wana utu na wakarimu karibu kwa mikoa yote 19 hadi 20 niliyowahi kutembelea wakati wa kutekeleza majukumu yangu”, alisema Bi. Maniza.
Alitoa wito kwa Serikali, kuendelea kutoa kipaumbele kwa ajili ya Sekta ya Elimu na Afya kwa kuongeza angalau asilimia moja ya bajeti kila mwaka kwakua zimekuwa na changamoto nyingi kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu kila siku.
Pia aliiomba Serikali ibuni mbinu na kuweka mipango endelevu kwa ajili ya watoto itakayowasaidia katika siku zijazo kwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa takriban watoto milioni 2 huzaliwa kila mwaka.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Isdor Mpango alimuahidi aliyekuwa Mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) Bi. Maniza Zaman, kuwa Wizara yake itaendelea kuhakikisha Sekta hizo zinapata bajeti ya kutosha katika mgawanyo.
Dkt. Mpango amemshukuru kwa kufanya kazi nchini na kumkaribisha tena na tena hasa kipindi cha mapumziko ambapo amesema milango ipo wazi muda wowote atakapojisikia kutembelea Tanzania.
Social Plugin