Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Tabora
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesisitiza marufuku yake aliyoitoa hivi karibuni kuhusu ajira kwa watoto ambao wapo chini ya miaka 18.
Mhe Hasunga amepiga marufuku hiyo leo tarehe 13 Mei 2019 wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa wa sekta ya Tumbaku katika hafla ya ufunguzi wa msimu wa masoko ya Tumbaku mwaka 2019 iliyofanyika katika maghala ya kampuni ya Alliance One Wilaya ya Urambo mkoani Tabora.
Alisema kuwa suala la ajira kwa watoto ni miongoni mwa mambo yanazuiliwa kwenye Sheria za kimataifa kupitia Shirika la Kazi Duniani (International Labour Organization) na Sheria za Ajira hapa nchini hivyo mdau yeyote atakayebainika kukiukwa maelekezo hayo atashtakiwa.
“Nawasihi wadau wote tuendelee kupiga vita ajira kwa watoto katika tasnia ya tumbaku kwa kuwa ni eneo ambalo limeendelea kulalamikiwa na wadau” Alikaririwa Mhe Hasunga
Kadhalika, Mhe Hasunga alisema kuwa katika kuhakikisha zao la tumbaku linaendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la mkulima na Taifa, Wizara imejiwekea malengo ya haraka yanayopaswa kutekelezwa ambayo ni pamoja na kukamilisha usajili wa wakulima wote wa tumbaku ifikapo tarehe 30 Juni 2019, kuwapatia vitambulisho na kuwaingiza kwenye kanzidata ili kupata takwimu za uhakika za maeneo wanayolima na kuiwezesha serikali kusimamia upatikanaji wa pembejeo kulingana na mahitaji yao.
Malengo mengine ni Tumbaku yote inayovunwa na wakulima sasa inauzwa ifikapo mwisho wa masoko tarehe 31 Julai, 2019 huku akiiagiza Bodi ya Tumbaku kushirikiana na wakulima wote kusimamia kwa makini masoko ili tuweze kuanza mapema maandalizi ya zao la msimu wa 2019/2020.
Aidha, mipango mingine ni kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati kwa kuweka utaratibu wa kumwezesha mkulima kujitegemea kwa pembejeo ili aache kuwa tegemezi wa mikopo ya mabenki yenye riba kubwa.
Mhe Hasunga ameiagiza Bodi na Tume ya Maendeleo Ushirika kuhakikisha wanavishirikisha wakulima kupitia vyama vyao kuweka akiba ya fedha kununua pembejeo kwa kukatwa kiasi watakachokubaliana wakati wa mauzo ya tumbaku.
Pamoja na malengo hayo ya haraka, Wizara ya Kilimo inasimamia utekelezaji wa malengo ya muda mrefu yakiwemo Upatikanaji wa wanunuzi wapya wa tumbaku kwa sasa na kwa miaka ijayo kabla ya Juni, 2020, Kuongeza ubora wa zao la tumbaku kutoka asilimia 87 ya sasa hadi asilimia 92 ifikapo Juni 2022 na Kuongeza mbegu mpya na bora za tumbaku ili tuweze kupata masoko katika nchi nyingine kama vile China.
Alisema ili kufikia malengo hayo wadau wote wa tasnia ya tumbaku wanapaswa kushirikiana ili kufikia malengo hayo na wakulima kunufaika na jasho lao.
“Viongozi ngazi ya Mkoa na Wilaya wakiwemo Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Waheshimiwa Wabunge, Wenyeviti wa Halmashauri na Wakurugenzi wa Halmashauri wanaowajibu na mchango mkubwa kuendeleza zao hili kwa kusimamia Sheria zinazosimamia zao hili, kusimamia huduma za ugani na kutenga fedha kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri” Alisisitiza Mhe Hasunga
Tumbaku ni miongoni mwa mazao makuu ya kimkakati ya yaliyopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mazao mengine ni pamoja na Tumbaku, Kahawa, Pamba, Korosho, Chai, michikichi na alizeti.
Mhe Hasunga alisema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa malengo ya uzalishaji yanafikiwa kwa kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, kuboresha huduma za ugani na kutafuta masoko mapya ya tumbaku.
Serikali inatumia mfumo wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja ili kuhakikisha mbolea inafika kwa wakati, kwa bei nafuu na kudhibiti upandishaji holea wa bei. “Nichukue nafasi hii kuigiza Bodi ya Tumbaku na viongozi wa vyama vya ushirika kuhakikisha kuwa wakamilisha kwa wakati kuweka malengo ya uzalishaji na mahitaji ya mbolea ili uagizaji wa mbolea ufanyike mapema” Alisema Mhe Hasunga
Takwimu zinaonesha kwamba kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 hadi kufikia mwaka 2016 tumbaku imekuwa na mchango mkubwa wa kuliingizia Taifa fedha za kigeni. Kwa mfano katika mwaka 2017, tumbaku iliingiza fedha za kigeni kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 195.8 ikishika nafasi ya pili baada ya zao la korosho. Licha ya faida kwa taifa, pia, uzalishaji wa tumbaku unawanufaisha wakulima, wanunuzi, viwanda vya kusindika tumbaku, mabenki, wasambazaji wa pembejeo, Halmashauri za wilaya na wadau wengine katika mnyororo wa thamani.
Social Plugin