Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA ARDHI YAANDAA MPANGO WA KUENDELEZA MAENEO YA UKANDA WA RELI YA KISASA YA STANDARD GAUGE (SGR)

Na Grace Semfuko,MAELEZO

Wizara ya ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi  inaandaa mpango maalum wa uendekezaji wa Ukanda wa reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) inayotoka Dar Es Salaam hadi Kigoma unaolenga kuwawezesha wakazi waishio kando ya Reli hiyo kunufaika kiuchumi kupitia ardhi zao kwa kufanya biashara zitakazopangwa kwenye maeneo hayo na ambazo wananchi wataamua kuzifanya.

Lengo la mpango huo  ni kutoa mwongozo wa namna matumizi ya ardhi yatakavyofanyika katika ukanda mzima wa SGR ambao utasaidia kuondoa matumizi yasiyokusudiwa na pia  utasaidia kuondoa migogoro ya adhi na kuibua fursa ambazo bado hazijajulikana na Wakazi wa maeneo hayo.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi wakati akizungumza na wakazi wa Vijiji vya Kwala na Soga vilivyopo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani kuhusu mpango bora wa matumizi ya ardhi kwenye ukanda wa Reli ya Kisasa ya SGR.

“Kila mahali kutakuwa na fursa za kiuchumi zinazopatikana mahali husika, haimaanishi tunaipanga ile ardhi ili ichukuliwe na serikali, hapana!  wananchi wenyewe watayatumia maeneo yao kwa mpango maalum,  tunataka wananchi wanufaike na ardhi yao” alisema Waziri Lukuvi.

Waziri Lukuvi aliwatoa hofu wakazi wa Maeneo yote ya SGR kuwa Serikali haina mpango na kuchukua ardhi zao na kuwataka pia kutouza ardhi hizo kwani tayari Serikali imeshazipandisha hadhi na thamani.

“Serikali inapanga matumizi bora ya ardhi yote katika Wilaya zote ambapo SGR inapita, tunataka kuwa na ukanda wa maendeleo ya kiuchumi , yaani mtu akifika hapa anajua kitu gani anakipata wapi, ukanda huu unaopitiwa na SGR sasa utapangwa rasmi, hatuwezi kuwa na reli ya kisasa yenye gharama kubwa kama hii lakini uendelezaji wa ardhi ni mbovu,mtu hataruhusiwa kufanya shughuli isiyoruhusiwa, hapa lazima ardhi ipangwe vizuri na tuwe na mpango mzuri  wa kiuchumi” alisema Lukuvi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi Immaculata Senje alisema pamoja na kuinua pato la wakazi waishio kando ya reli hiyo mpango huo pia unalenga kulinda mazingira na kupendezesha maeneo hayo na wameshaanza maandalizi ya awali ya kukusanya taarifa za mpango huo.

 “Utakuwa ni mpango shirikishi kuanzia ngazi za vijiji hadi Taifa, mpaka sasa timu ya wataalamu imeundwa na imeshaanza maandalizi ya awali kwa kukusanya taarifa muhimu ambazo zitasaidia kuutekeleza mpango huu, tutafanya kazi na wote, lengo la mpango huu ni kutoa mwongozio wa namna matumizi ya ardhi yatakavyofanyika katika ukanda mzima” alisema Senje


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com