TIMU ya Zamalek ya Misiri imefanikiwa kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa penalti 5-3 kufuatia sare ya jumla ya 1-1 dhidi ya Renaissance Sportive Berkane, maarufu kama RSB Berkane usiku wa jana Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
Bao pekee la penalti la beki Mmisri, Mahmoud Alaa Eldin dakika ya 55 liliipa Zamalek ushindi wa 1-0 ndani ya dakika 120 za mchezo wa jana Misri.
Na kufuatia RSB Berkane kushinda 1-0 pia, bao pekee la mshambuliaji Mtogo, Fo-Doh Kodjo Laba dakika ya 90 na ushei akimalizia pasi ya Hamdi Laachir liliipa RSB Berkane Uwanja wa Manispaaa ya Berkane Mei 20 mchezo ukahamia kwenye mikwaju ya penalti.
Zamalek ilipata penalti zake zote kupitia kwa nyota wake, Mmorocco mzaliwa wa Ufaransa, Khalid Boutaib, Mahmoud Alaa, Abdallah Gomaa, Youssef Obama na Ahmed Sayed ‘Zizo’.
Lakini Hamdi Laachir akakosa penlati ya kwanza ya Berkane, wakati Ismail Mokadem, Mtoto Fo-Doh Kodjo Laba na Mburkina Faso, Issoufou Dayo walifunga.
Jana ilikuwa mara ya nne katika fainali 16, mikwaju ya penalti inaamua mshindi wa taji hilo, timu nyingine zilizowahi kutwaa Kombe hilo kwa matuta ni Hearts of Oak ya Ghana, Stade Malien ya Mali na MAS Fes ya Morocco.
Ushindi huo unamaliza ukame wa mataji ya Afrika wa miaka 16 kwa Zamalek mara ya mwisho wakishinda mwaka 2003 taji la Ligi ya Mabingwa ambalo walivuliwa na Simba SC ya Tanzania.
Wapinzani wao wa Jiji la Cairo, Al Ahly wanaongoza kwa kutwaa mataji mengi Afrika, 19 wakifuatiwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mataji 11.
Kwa ushindi huo, Zamalek watapatiwa dola za Kimarekani Milioni 1.25, huku Berkane wakiambulia dola 625,000.
'The White Knights' sasa watamjua mpinzani wao kwenye kuwania taji la Super Cup ya CAF 2019 wiki ijayo wakati Esperance ya Tunisia itakapomenyana na Wydad Athletic ya Morocco kufuatia kutoa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza mjini Rabat.