Msemaji Mkuu wa serikali ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo, Dkt. Hassan Abbas, (kushoto), akipeana mikono na Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF), Bi. Eunice Chiume baada ya mazungumzo yao ofisini kwa Dkt. Abassi jijini Dar es Salaam leo Juni 15, 2019. Bi. Chiume ambaye alikuwa katika ziara ya kuvitembelea vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii jijini Dar es Salaam, amehitimisha ziara hiyo kwa kufanya mazungumzo na Dkt. Abbas.
Dkt. Abbas (kulia), akimsikiliza mgeni wake. Bi. Eunice Chiume ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Bi. Chiume akiziungumza.
Dkt. Abbas (kulia), akijadiliana jambo na Bi. Eunice Chiume, (katikati), na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi ,mara baada ya mazungumzo yao.
Msemaji Mkuu wa serikali ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo, Dkt. Hassan Abbas, (kushoto), akipeana mikono na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa PSSSF bw. Abdul Njaidi.
Dkt. Abbas akiwa na wageni wake, Bi. Eunice Chiume (katikati) na Bw. Abdul Njaidi kutoka PSSSF.
***
NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
MSEMAJI Mkuu wa serikali, Dkt. Hassan Abbasi ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuanza vizuri kutekeleza majukumu yake katika kipindi kifupi tangu kuunganishwa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Dkt. Abbas ameyasema hayo leo Jumamosi Juni 15, 2019 ofisini kwake jijini Dar es Salaam wakati alipotembelewa na Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma, (PSSSF), Bi. Eunice Chiume, aliyefuatana na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko huo Bw. Abdul Njaidi.
Kwa takriban wiki nzima, Meneja huyo amekuwa kwenye ziara ya kuvitembelea vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii ili kujenga mahusiano ikiwa ni pamoja na kueleza malengo ya Mfuko huo ambao ni mpya baada ya serikali kuunganisha Mifuko minne ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF, LAPF, PPF na GEPF kwa lengo la kuboresha utoaji huduma.
“Tunaposikia kuwa watu wameanza kupata mafao yao tena kwa wakati kwakweli ni jambo la faraja kwa serikali kwa hiyo mpeleke salamu zangu kwa watendaji wote, akiwemo mtendaji mkuu wa Mfuko, tunafarijika sana tunapoona kwamba yale malengo ya serikali kuu kuunganisha hii mifuko ili kutoa huduma bora yametimia.” Alisema.
Dkt, Abbas ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo, pia amempongeza Meneja huyo kwa uamuzi wa kuvitembelea vyombo vya habari kwa lengo la kuelimisha umma na kueleza shughuli za Mfuko kwani hii itasaidia wanachama kujua kinachoendelea kwenye Mfuko wao.
“Huu ni Mfuko mpya, yako maswali mengi yanayozua tashtiti na tashwishwi ambavyo kwa pamoja vinafanya kitu kinaitwa jakamoyo ambayo ni vile mtu anaumia moyoni kumbe anakuwa tu hana taarifa sahihi, hili nalo niwapongeze baada ya kukamilisha zile taratibu za ndani na kuhakikisha wale wastaafu wanapata kile kilicho chao sasa kazi kubwa ni kutoa elimu.” Amefafanua Dkt, Abbas.
Aidha Dkt. Abbasi alitoa wito kwa wastaafu na wale wastaafu watarajiwa kutambua kuwa msingi wa pensheni ni kumuhudumia mfanyakazi anapokosa nguvu ya kufanya kazi, ama uzeeni au kutokana na kupata madhara mengine ambayo yatafanya akose nguvu ya kufanya kazi.
“Niwakumbushe watanzia kuwa tuweke pesa benki zile tunazohitaji kutumia leo, kesho au katika kipindi kifupi, lakini mafao ni kwa ajili ya kukusaidia katika maisha ya baadaye, si vema umetumikia nchi, jamii halafu baada ya kustaafu ukaishi maisha ya mashaka.” Aliasa.
Awali Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma wa PSSSF, Bi. Eunice Chiume alimweleza Dkt. Abbas kuwa amepata fursa ya kutembelea vyombo vya habari ili kujenga na kuendeleza mahusiano ikiwa ni pamoja na kuutambulisha Mfuko huo mpya kwa wadau wa sekta ya habari.
Alisema Mfuko ulianza kutekelez amajukumu yake Agosti 1, 2018 na ndani ya miezi 6 tangu Mfuko uanze kutekeleza majukumu hayo umeweza kulipa malimbikizo ya pensheni ya mkupuo na ile ya kila mwezi kiasi cha shilingi bilioni 880, lakini pia Mfuko unaendelea na zoezi la kuhakiki taarifa za wanachama (wastaafu) ambapo kati ya wastaafu 120,000, elfu 10,000 bado hawajahakikiwa.
“Kwa hiyo tumeeleza kuwa Mfuko umefungua ofisi nchi nzima bara na visiwani na kwa kila mstaafu ambaye bado hajahakiki taarifa zake afike kwenye ofisi ya PSSSF iliyo karibu naye ili atekeleze wajibu huo wa kisheria.” Alifafanua Bi. Chiume.
Social Plugin