Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : AGAPE,KIWOHEDE WAFUNGA MRADI WA ELIMU YA AFYA YA UZAZI NA UJINSIA KWA VIJANA





Mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Shinyanga AGAPE ACP na KIWOHEDE, wamehitimisha mradi wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana, ambao ulilenga kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ili wanafunzi waweze kutimiza ndoto zao.



Kikoa cha kufunga mradi huo wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana, kimefanyika leo Junei 25, 2019 kwenye ukumbi wa mikutano wa hotel ya Vigimark  mjini Shinyanga, na kuhudhuriwa na walimu,wanafunzi, maofisa ustawi wa jamii, elimu, madiwani, watendaji wa kata, viongozi wa kidini, kimila pamoja na wataalamu wa afya.

Utekelezaji wa mradi huo wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia ulianza mwaka 2017 na kuhitimishwa Juni 30 mwaka huu (2019), ambapo Shirika la A GAPE lilikuwa likiutekeleza kwenye kata ya Usanda halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, huku shirika la KIWOHEDE waliutekeleza katika kata ya Zongomela halmashauri ya Kahama Mji kwa ufadhili wa Shirika la Sida kupitia Save the Children.

Akizungumza wakati wa kufunga  mradi huo, mgeni rasmi Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Rashid Mfaume kwa niaba ya katibu tawala wa mkoa huo Albert Masovela, aliyapongeza mashirika hayo mawili kwa kazi nzuri ambayo wameifanya ndani ya jamii kwa kutetea haki za watoto katika kutokomeza mimba na ndoa za utotoni.


Alisema mashirika hayo yamekuwa na mchango mkubwa sana ndani ya jamii, katika kutoa elimu hiyo ya elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana, kwa kusaidia vijana kuwapatia elimu ya kujitambua pamoja na wazazi kutambua umuhimu wa elimu, na athari za kuwaozesha wanafunzi ndoa za utotoni.

“Serikali tunayapongeza sana mashirika haya yasiyo ya kiserikali Agape pamoja na Kiwohede, kwa kazi nzuri ambayo mmekuwa mkiifanya ndani ya jamii hasa kwenye mradi wenu huu wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana, ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la mimba na ndoa za utotoni,”alisema Dkt. Mfaume.


“Nilikuwa natoa ombi kwa wafadhili wa mradi huu wauendeleze na kwenye kata zingine ili tuweze kutokomeza kabisa tatizo hili la mimba na ndoa za utotoni, ambapo katika mkoa wetu wa Shinyanga bado tunaongoza kwa mimba na ndoa za utotoni kwa asilimia 59 kwa takwimu za mwaka 2012,”aliongeza.

Naye mkurugenzi wa Shirika la AGAPE, John Myola alisema waliuanzisha mradi huo mara baada ya kufanya utafiti mdogo mwaka 2016 na kubaini kuwepo na tatizo kubwa la wanafunzi kupewa ujauzito na ndoa za utotoni na hatimaye kuzima ndoto zao.


Nao maofisa elimu wa kata ya Usanda,halmashauri ya Shinyanga na Zongomela Kahama Mji, wamekiri mashirika hayo yamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la mimba na ndoa za utotoni tofauti na miaka ya nyuma hali ilivyokuwa.


Akitoa takwimu za mimba shuleni, afisa elimu wa kata ya Usanda Sospeter Kasonta, alisema mwaka 2017 kulikuwa na mimba 11, 2018 4 na mwaka huu 2019 Januari hadi Juni kuna mimba moja.


Aidha afisa elimu kata ya Zongomela halmashauri ya Kahama Mji Matonelo Mwagala, naye ametoa takwimu za mimba kuwa mwaka (2017) kulikuwa na mimba tatu, (2018) moja, na (2019) Januari hadi June kuna mimba moja.

Na Marco Maduhu - Malunde1 blog
TAZAMA PICHA HAPA CHINI


Mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Rashid Mfaume afunga wa mradi wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kwa niaba ya katibu tawala wa mkoa wa Shinyanga Albert Msovela. Dkt. Mfaume aliyapongeza mashirika ya AGAPE  na KIWOHEDE kwa kazi nzuri wanayoifanya ndani ya jamii, na kuahidi serikali itaendelea kushirikiana nayo ili kuendelea kuleta ukombozi wa watoto wa kike na kuweza na kutimiza ndoto zao. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la AGAPE ,John Myola akielezea namna walivyoanzisha mradi wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana ,ambao ulilenga kutokomeza mimba na ndoa za utotoni na sasa umefikia kikomo, ambapo umeleta mabadiliko makubwa kwa kupunguza mimba za wanafunzi na kutokomeza ndoa za utotoni.

Mratibu wa mradi wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Sida kupitia Save The Children John Komba, akielezea kuridhishwa na mashirika hayo ya KIWOHEDE na AGAPE namna walivyoutendea haki mradi huo kwa kupunguza matukio ya mimba na ndoa za utotoni katika kata ya Usanda Shinyanga na Zongomela Kahama Mji.

Mratibu wa mradi wa elimu ya afya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la AGAPE Lucy Maganga akielezea namna walivyokuwa wakiutekeleza mradi huo, kwa kushirikisha wanafunzi, walimu, wazazi, wazee maarufu, wa kimila ,viongozi wa kidini, watendaji wa Kata, vijiji na vitongoji, maofisa maendeleo na ustawi wa jamii, na hatimaye kufanikiwa kupunguza tatizo ka mimba na ndoa za utoto kwenye kata hiyo ya Usanda.

Mratibu wa mradi wa elimu ya afya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la Agape Lucy Maganga, akielezea changamoto ambazo walikutana nazo kwenye utekelezaji wa mradi huo, kuwa ni jamii kuendekeza mila na desturi kandamizi za kutomthamini mtoto wa kike na kumuozesha ndoa za utotoni ili wazazi wapate mali na mifugo, ambapo kwa sasa ndoa za utotoni hazipo tena.

Afisa mradi wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kwa vijana kutoka Shirika la KIWOHEDE wilayani Kahama Amos Juma, akielezea namna mradi huo walivyokuwa wakiutekeleza kwenye kata ya Zongomela halmashauri ya Kahama Mji, ambapo kwa sasa wameukabidhi rasmi serikalini ili kuendeleza na mapambano ya kutokomeza mimba na ndoa za utotoni na kubaki kuwa historia tu.

Afisa miradi kutoka Shirika la Agape Peter Amani akielezea namna sheria ya ndoa ya mwaka 1971, ilivyo kikwazo katika mapambano ya kutokomeza mimba na doa za utotoni, ambapo ina ruhusu mtoto mwenye umri wa miaka 14 kuolewa kwa ridhaa ya wazazi na miaka 15 ridhaa ya mahakama.

Mtendaji wa Kata ya Usanda Shinyanga, Emannuel Maduhu akizungumza kwenye kikao hicho, amelipongeza Shirika hilo la Agape kwa kutekeleza mradi huo kwenye kata yake ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza mimba za wanafunzi tofauti na hapo awali, huku ndoa za utotoni zikikoma kabisa.

Diwani wa kata ya Usanda Foresta Nkole, naye amelipongeza Shirika hilo la Agape kwa kazi kubwa waliyoifanya kwenye kata yake ya kutokomeza ndoa za utotoni ambapo na yeye alikuwa ni miongoni mwa washiriki wa ndoa hizo , na kuahidi kuendeleza mapambano ya kuzipinga licha ya Agape mradi wao kukoma, ili wanafunzi wa kike waweze kutimiza ndoto zao.

Mwalimu kutoka Shule ya msingi Shingida Kata ya Usanda Costantine Maaro, akielezea namna Shirika la Agape lilivyo saidi wanafunzi kujitambua na kuweza kutoa hata taarifa za matukio ya ukatili na kuweza kukomeshwa kabla ya kuleta madhara.

Mwanafunzi kutoka shule ya msingi Zangaluba kata ya Usanda, Oliva Paschal, akielezea namna Shirika la Agape lilivyowasaidia kujitambua, kujiamini na kuweza hata kupinga matukio ya unyanyasaji dhidi yao likiwamo suala la kutaka kuozeshwa ndoa za utotoni.

Mtedaji wa kata ya Zongomela halmashauri ya Kahama Mji Yasinta Kimario, akielezea namna shirika la Kiwohede lilivyosaidia kupunguza matukio ya mimba na ndoa za utotoni kwenye kata hiyo tofauti na hapo awali hali ilikuwa ni mbaya.

Afisa elimu wa Kata ya Zongomela halmashauri ya Kahama Mji Matonelo Mwagala, akielezea namna Shirika la KIWOHEDE lilivyosaidia kupunguza mimba za wanafunzi mashuleni, ambapo mwaka (2017) kulikuwa na mimba tatu, (2018) mimba moja na mpaka sasa (2019) kuna mimba moja.

Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari Isunuka kata ya Zongomela halmashauri ya Kahama Mji Neema Steven, akielizea namna Shirika la KIWOHEDE, alilivyowasaidia kuwapatia elimu ya kujitambua, pamoja na kuweza kupasa sauti za kudai haki zao kupitia kwenye klabu yao ya Tuseme shuleni hapo na kuweza kutatua changamoto zinazowakabili.

Jackline Ghuba ni mwanafunzi aliyehitimu elimu ya Sekondari katika Shule ya Isanuka, akielezea namna Klabu ya Tuseme, iliyoanzishwa na Shirika la KIWOHEDE Shuleni hapo na kusaidia kupata elimu ya kujitambua na kumaliza masomo yake bila ya kupewa ujauzito wala kuozeshwa ndoa za utotoni.

Afisa Muuguzi kutoka hospitali wilaya ya Kahama Nyanjura Mjuberi, akielezea Shirika la KIWOHEDE namna lilivyosaidia kupuguza idadi ya watoto waliochini ya umri wa miaka 18 kumimika hospitali hapo kwa ajili ya kujifungua ambapo mwaka (2017), walikuwa wanafika 664, (2018) wakapungua na kufika 416 na mwaka huu (2019) Januari hadi Machi wamefika 91.

Wadau wakiwa kwenye kikao cha kuhitimishwa mradi wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka Shirika la Agape na KIWOHEDE na kuukabidhi rasmi serikalini.

Kikao kikiendelea.

Kikao kikiendelea.

Kikao kikiendelea.

Wadau wakiendelea na kikao.

Wadau wakiendelea na kikao.

Kikao kikiendelea.

Wadau wakiwa kwenye kikao cha kuhitimishwa mradi wa elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka Shirika la Agape na KIWOHEDE na kuukabidhi rasmi serikalini.

Afisa ustawi wa jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Elizabeth Mweyo akiongoza mjadiliano nini kifanyike ili kuendelea mapambano ya kutomeza mimba na ndoa za utotoni kwenye kata hizo za Usanda na Zongomela licha ya mashirika hayo mradi wao kuhitimishwa na kukubaliana elimu iendelee kutolewa pamoja na wahusika wanaowapa mimba wanafunzi na kuwaozesha ndoa za utotoni wakamatwe na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Washiriki wa kikao wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Na Marco Maduhu- Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com