Wafanyakazi wawili wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Songwe wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari waliyokuwa wamepanda kugongana na lori maeneo ya Izazi kata ya Izazi tarafa ya Ismani wilaya ya Iringa na mkoa wa Iringa katika barabara kuu ya Iringa-Dodoma.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa ACP Juma Bwire Makanya ajali hiyo imetokea Juni 25,2019 majira ya saa 11 na dakika 45 alfajiri ambapo gari lenye namba za usajili STL 3807 aina ya toyota Hilux mali ya TARURA ikiendeshwa na Lodrick Richard Ulio( 35) mkazi wa Dar es salaam likitokea Iringa kuelekea Dodoma liligongana uso kwa uso na gari lenye namba za usajili T 146 BAZ aina ya Mitsubishi fuso mali ya Wilson Msenga wa Iringa likiendeshwa na Amos wa iringa likitokea Dodoma kuelekea Iringa.
Kamanda Makanya amewataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni Lodrick Richard Ulio (dereva wa TARURA) na Joyce Enezar Mlay (45) ambaye ni mkazi wa Moshi na majeruhi kuwa ni Ernest Mgeni (49) mkazi wa Mbozi, Gervas Myovela (44) mkazi wa Mbozi na Jamadin Mikata( 32) mkazi wa Mbozi wote wakiwa ni wafanyakazi wa TARURA mkoa wa Songwe na wamehamishiwa hospitali ya rufaa Iringa kwa matibabu.
Amesema miili ya marehemu imekabidhiwa kwa meneja wa TARURA Manispaa ya Iringa na kupelekwa Dodoma tayari kwa utaratibu wa mazishi.
“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa fuso kushindwa kulimudu gari lake na kusababisha kuhama upande mmoja na kugongana uso kwa uso ambaye amekimbia mara baada ya ajali hiyo na anatafutwa",ameeleza Kamanda.
Kamanda Makanya ametoa wito kwa madereva wawe makini wanapotumia barabara wasijione wako peke yao bali waheshimu sheria na watumiaji wengine wa barabara.
Na Mwandishi wa Malunde 1 blog - Iringa
Na Mwandishi wa Malunde 1 blog - Iringa
Social Plugin