Msimamo wa Asasi za Kiraia kuhusu Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali, Juni 2019
Mnamo Jumatano Juni 19, 2019 asasi za kiraia kama sehemu ya wadau katika kuchangia mabadilko ya sera na sheria mbalimbali zilipokea mapendekezo ya marekebisho ya sheria nane tofauti ambapo mapendekezo hayo yameplekwa kwa Kamati ya Bunge ya katiba na Sheria kwa hati ya dharura.
Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Makampuni, Sheria ya Asasi za Kiraia, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Vyama vya Kijamii, Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza pamoja, Sheria ya Wakala wa Usafirishaji Majini, Sheria ya Hatimiliki na Sheria ya Miunganiko ya Wadhamini. Mabadiliko haya yanapendekezwa kufanywa kwa haraka kutumia taratibu ambazo kwa kawaida hufuatwa pale panapokuwa na jambo la dharura.
Kwa ujumla, mabadiliko yanayopendekezwa katika sheria hizo yanalenga kudhibiti utendaji kazi wa asasi za kiraia hivyo kuathiri namna wananchi wanavyoweza kutumia haki yao ya kujumuika, kushirkiana, kuwekeza, kueleza maoni yao kwa uhuru, haki ya kushiriki katika uchumi na maamuzi yanayowaathiri na kuwawajibisha viongozi wao.
Asasi za kiraia
Asasi za kiraia ni mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayofanya kazi kwa maslahi ya wananchi. Kwa kiwango kikubwa asasi za kiraia zimefanikisha mengi katika kukuza ustawi wa watu na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Mchango wa asasi za kiraia
Asasi za kiraia zinachangia mambo mbali mbali nchini ikiwa ni pamoja na:
- Kutoa huduma za kijamii – asasi za kiraia zinatoa huduma za moja kwa moja ikiwemo huduma za afya mfano kutoa dawa na huduma nyingine za matibabu ikiwemo kwa waathirika wa UKIMWI na magonjwa mengine. Kwa mujibu wa ripoti ya idara ya maendeleo ya Jamii juu ya mchango wa Azaki kwenye maendeleo nchini, asasi hizi zina mchango mkubwa sana kwenye sekta ya afya, elimu, Kilimo, nishati, utawala bora, mazingira na maendeleo ya jinsia.
- Wakati mwingine katika jukumu hili, asasi za kiraia hufanya kazi moja kwa moja na serikali, kusaidia kujenga vituo vya afya vya serikali, vyanzo vya maji, na shule.
- Mashirika ya kiraia yanasaidia serikali kupata maoni juu ya maamuzi na vitendo vyake, ama kutoka kwa shirika au kwa kukusanya maoni kutoka kwa vikundi tofauti katika maeneo tofauti.
- Mashirika ya kiraia mara nyingi husaidia kuibua mawazo mapya na suluhu ya matatizo ambayo wanaweza kuyafanyia majaribio kabla ya kushauri serikali kutekeleza. Mfano mmoja wapo ni ubunifu uliofanyika katika sekta ya elimu katika kuainisha namna bora za kuhamasisha walimu kuhakikisha wanafunzi wanajifunza na kufaulu vema zaidi. Katika sekta ya afya, asasi za kiraia nchini zimekuwa na mchango mkubwa katika uvumbuzi wa maambukizi ya ugonjwa wa Malaria ambao unatumika kuboresha sera na mipango ya serikali.
- Asasi za kiraia hufanya kazi ya kujenga misingi ya usawa katika jamii kwa kuwalinda na kuwatetea watu wenye mahitaji maalumu na wanyonge.
- Mashirika ya kiraia hutusaidia kujifunza, yanazalisha ujuzi mpya na kushirikiana na wananchi na viongozi ili iweze kuchangia maendeleo.
- Mashirika ya kiraia huajiri maelfu ya watu, hulipa mamilioni ya shilingi kama kodi na huchangia mamilioni ya shilingi kwa uchumi wa ndani kwa kununua bidhaa na huduma mbalimbali.
Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria hizi yanatishia ustawi wa asasi za kiraia kwa sababu kuu zifuatazo:
Marekebisho haya yatabatilisha kazi nzuri na za msingi zinazofanywa na asasi za kiraia
Marekebisho ya Sheria ya Makampuni, Sheria ya Vyama vya Kijamii, Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali na Sheria ya miunganiko ya Wadhamini yanaweka masharti kwamba shirika lolote linalofanya kazi za maendeleo haliziwezi tena kusajiliwa kama kampuni isiyotengeneza faida (Marekebisho ya 4,5,6). Katika mabadiliko ya Sheria ya Asasi za Kiraia tafsiri ya asasi za kiraia haijitoshelezina yamejikita kuweka zuio la aina ya shughuli zinazokufanyika na asasi tofauti na haki ya raia kujumuka inayopatikana kwenye ibara ya 20 ya Katiba yetu ya mwaka 1977 (Marekebisho 25). Asasi yoyote ambayo itakuwa haijasajaliwa chini ya sheria sahihi kwa mujibu wa tafsiri mpya ya zitapaswa kuomba usajili – bila kuzingatia kama asasi hizo zimesajiliwa na zimekuwa zikifanya kazi tayari, ni taasisi halali ambazo zimeajiri watu, zinalipa kodi na zinatoa mchango mkubwa kwa jamii na nchi. (Marekebisho 28, 36). Kinyume chake, asasi zinapewa muda wa miezi miwili kuhakikisha zinatekeleza masharti ya sheria mpya (Marekebisho 6). Hata mashirika ambayo tayari yana cheti cha usajili chini sheria ya Asasi za Kiraia yanaweza kufutiwa usajili kama hayatatekeleza matakwa ya sheria mpya (Marekebisho 28)
Athari za kiuchumi na kijamii zitakazotokana na vikwazo kwa asasi za kiraia
Endapo marekebisho haya yatapitishwa kama yalivyo, mashirika mengi ya kiraia yatafutiwa usajili na kushindwa kuanza tena. Kwa kufanya hivyo kuna madhara kadhaa yatajitokeza ikiwemo; watu kupoteza ajira, watoa huduma kukosa mapato, serikali kupoteza mapato ya kodi (kodi za mapato na kodi za utendaji, pamoja na kodi zinazotokana na bidhaa na huduma zinazotumiwa na mashirika hayo). Pia kuna mashirika mengi yanayotoa huduma mbalimbali, kujenga uwezo, na kutoa rasilimali ambapo wanufaika wake watakosa huduma hizo.
Marekebisho haya pia yanaweka vikwazo vikubwa kwa watengeneza filamu wa kimataifa (Maarekebisho 17 na 21) ambayo yanalenga kudhibiti matumizi ya mandhari pamoja na maudhui ya filamu nchini Tanzania. Hii inaibua hatari kubwa ya kuwafanya watengeneza filamu kuchagua maeneo mengine ya kufanyia filamu na kuiepuka Tanzania hasa pale watakapokumbana na urasimu usio wa lazima. Hivi karibuni, Afrika Kusini wameingia makubaliano na Kenya kutoa msaada wa kiufundi katika kufundisha lugha ya Kiswahili. Je, kuna uwezekano kwamba fursa hii haikuletwa Tanzania kwa sababu ya kukithiri kwa urasimu? Marekebisho haya pia yanaonekana kukinzana na msimamo wa serikali wa kujenga mazingira rafiki kwa kupunguza urasimu katika uratibu wa sekta binafsi.
Kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha udhibiti, mamlaka makubwa wanayopewa maafisa na tafsiri kandamizi zilizopo katika marekebisho haya, yanaweza kusababisha mgongano na jamii ya kimataifa na kupelekea kuharibu taswira ya nchi. Badala yake tunapaswa kushirikiana kuhakikisha tunafanyia kazi marekebisho haya kwa umakini ili kuweka mizania muhimu kuhakikisha kuwa majukumu ya Msajili mbali na kudhibiti pia yanakuwa wezeshi kwa asasi za kiraia. Maoni haya pia yanakusudia kuepusha athari kwa shughuli za kitalii na vyanzo vingine vya mapato ambavyo vinategemea mapato kutoka nje ya nchi.
Mianya mipya ya kuchuja taarifa
Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ni mapana sana kiasi cha kuweka vikwazo hususani katika maudhui ya picha za video.
Majukumu ya Bodi ya Filamu (Marekebisho 18) ni mapana na yanajumuisha kudhibiti, kufuatilia, kutoa vibali, kuidhinisha na kusimamia. Majukumu haya yote hayajafafanuliwa kwa ufasaha hivyo kutoa mamlaka yasiyodhibitiwa kwa Bodi ya Filamu katika kusimamia maudhui.
Pendekezo la 20 linatoa mamlaka yasiyo ya kawaida ya kudhibiti maudhui, ikisisitiza kwamba kila bango litakaloandaliwa na kubandikwa hadharani linapaswa kupitiwa na kuidhinishwa na Bodi ya Filamu.
Kukosekana kwa usawa na kutokufuatwa kwa misingi ya utoaji haki
Msajili na Waziri ni watueliwa wa Rais, waajiriwa na serikali na wanawajibika kwake kwa mujibu wa Katiba yetu. Wakati huo huo, wanapewa mamlaka ya kufanya maamuzi ya haki na yasiyo ya kibaguzi katika kufungia mashirika. Msajili anapewa majukumu ya kushutumu na kuhukumu, kinyume na misingi ya asili ya haki. Kwa kuzingatia kile anachokiamini, kwa mfano kuhusu kampuni inayojihusisha na masuala ya kijinai, Msajili anaweza kuiandikia barua na kufikia maamuzi kwamba hajaridhishwa na majibu ya kampuni hiyo na kuifutia usajili kampuni hiyo (Marekebisho 10). Kwa mujibu wa Marekebisho, hakuna haja ya kutatua mashauri haya katika mahakama yoyote au vyombo vingine vya maamuzi. Kampuni inaweza kutafuta suluhu mahakamani ikiwa tayari imeshafungiwa. Hii ni kinyume na misingi ya haki ya asili ambayo ipo kwa mujibu wa sheria za nchi.
Vile vile, Marekebisho ya 26 ya Sheria ya Asasi za Kiraia yanamuongezea mamlaka mawili Msajili wa Asasi za Kiraia: mamlaka ya kusimamisha asasi na mamlaka ya kufanya uperembaji wa asasi kila baada ya miezi mitatu. Hata hivyo, hakuna sababu yoyote ya msingi inayotajwa kuthibitisha mamlaka hayo mapana. Tayari kwa sharia ya sasa namba 24 ya mwaka 2002 asasi zinawajibika kuwasilisha ripoit hizi pamoja na hesabu za mwaka na fomu namba 10% inayokusanya taarifa zote za msingi kuhusu asasi hizi.
Uhai wa mashirika yaliyosajiliwa chini ya Sheria ya Vyama vya Jamii, uko chini ya matakwa ya Waziri. Marekebisho ya 38 yanatoa mamlaka kwa upande wa Waziri kufuta chama cha kijamii kwa kuwa tishio kwa utawala bora wa nchi. Kwa mujibu wa sheria za Tanzania na marekebisho yanayopendekezwa, vyama vya kijamii nchini ni pamoja na taasisi mbali mbali za kidini zilizosajiliwa chini ya sheria ya Vyama vya Kijamii ya mwaka 1954.
Kuweka vikwazo katika historia ndefu na yenye manufaa katika kujumuika na kushirikiana
Watanzania wana historia ndefu ya kujumuika, kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja, hususani katika mifumo isiyo rasmi. Marekebisho haya yanaweza kuathiri historia hii kwa kiasi kikubwa. Mashirika mengi nchini yatapata shida kufikia vigezo vipya vilivyowekwa ili kujisajili au yatashindwa kufanikisha usajili katika muda mchache uliwekwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao. Urasimu pia unaweza kukatisha tamaa mashirika mapya kuanza. Kwa kiwango kikubwa hii itaathiri uwezo na utayari na nafasi ya jamii na kupelekea wananchi kushindwa kujumuika. Sheria ya Maudhui Mtandaoni (2018) imeleta hali hii kwa waandishi wa habari za mtandaoni (bloggers): blogu nyingi zilifungwa mara baada ya kutungwa kwa sheria hiyo, wengine waliomba usajili wakijua malipo ya ada yatalipwa kwa awamu na baadae wakashindwa kuendelea baada ya kutakiwa kulipa kwa mara moja. Blogu nyingi sasa zimefungwa nchini Tanzania na kusababisha vijana wengi sana kupoteza ajira na mapato. Marekebisho yanayopendekezwa yana hatari ya kuleta madhara makubwa kwa wengi wanaofanya kazi katika mashirika haya lakini zaidi kwa Jamii inayofaidika na huduma za asasi hizi.
Kunyamazisha sauti za wananchi, kupelekea kutokuridhika
Chini ya Marekebisho haya, wananchi watakuwa na nafasi finyu na kukosa njia mbadala za kutatua changamoto zao endapo njia zao za kawaida zitashindikana. Asasi za kiraia zinatoa mchango muhimu katika kuchambua na kupaza sauti za wananchi katika michakato ya kuandaa sera, kuelezea malalamiko, au kuwawezesha kujifunza zaidi kuhusu masuala mbalimbali; asasi za kiraia husaidia kujenga uelewa juu ya taarifa muhimu za serikali; pia asasi za kiraia huwezesha ushiriki wa wananchi. Mashirika mengi yanayofanya kazi hii yapo katika hatari ya kufutiwa usajili. Hii inaweza kupelekea hali ambayo wananchi watajiona wanakosa nafasi ya kueleza changamoto na masuala yao na kuja pamoja kuzitatua, na kuwafanya wajihisi kutengwa na kutokuwa na nguvu katika kufanya maamuzi ya wanayowahusu.
Kwa ujumla, asasi za kiraia tunaamini kwamba ni muhimu serikali kuratibu mashirika yote nchini, na hii ni sehemu muhimu ya kazi za serikali. Lakini tunapaswa kufanya mabadiliko kwa uangalifu na kwa kutafakari kwa kina, ili kuweza kufanya maamuzi sahihi. Vinginevyo, tunaweza kuwa na nia njema lakini tukajikuta tunafanya makossa na kupelekea madhara yasiyotarajiwa ambayo yanaweza kuchukua miaka mingi kurekebisha.
“Tunapendekeza kuwepo kwa muda wa kutosha kwa wadau/wananchi kuyajadili Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria hizi na kutoa maoni yatakayosaidia kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza”
Imetolewa Juni 22, 2019 na:
- Centre for Strategic Litigation
- Change Tanzania
- Equality for Growth
- HakiElimu
- Haki za Raia Tanzania
- JamiiForums
- Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
- Policy Forum
- Save the Children
- Tanzania Gender Network Program (TGNP)
- Tanzania Human Rights Defenders Coalition(THRDC)
- Tanzania Women Lawyers Association (TAWLA)
- TIBA
- Twaweza
#UhuruWetu
--
Risha Chande
Director of Engagement and Advocacy
Twaweza
m: +255 (0) 656 657 559
o: +255 (0) 22 2664301 - 3
f: Twaweza Tanzania
t: @Twaweza_NiSisi