Mkazi wa Kijiji cha Majengo, Kata na Tarafa ya Mtama, Wilaya ya Lindi Ramadhani Haji Juma, amehukumiwa kwenda gerezani kutumikia kifungo cha miaka 30, baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na madawa ya kulevya aina ya Bangi yenye uzito wa Kilo 7.8 kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Lindi, Liliani Rugalabamo,baada ya Mshtakiwa kukiri kosa lililomkabiri bila ya kulazimishwa.
Baada ya mshitakiwa kukiri kosa, Hakimu Rugalabamo alimuuliza mshtakiwa kama anazo sababu zitakazoishawishi Mahakama isimpe adhabu kali, Ramadhani Haji Juma aliomba asipewe adhabu kali, akidai ni mkosaji wa mara ya kwanza na alilazimika kujiingiza kwenye Biashara hiyo kwa lengo la kujipatia riziki ya kila siku.
"Mh,Hakimu naiomba Mahakama yako tukufu inisamehe na sitarudia kufanya kosa la aina hii tena kushiriki kazi hii "Amesema Ramadhani.
Kufuatia utetezi huo, hakimu Rugalabamo alirejea kwa Mwanasheria wa Serikali, Yahaya Gumbo iwapo anazo kumbukumbu za makosa ya zamani kwa mshtakiwa na kujibu hana, huku akiiomba mahakama impatie adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine walio na tabia ya aina hiyo.
Hakimu Rugalabamo akimpatia mshitakiwa adhabu katika kesi hiyo Namba 41/2019, alipinga utetezi huo kwa kusema hauna mashiko, kwani zipo njia nyingi za halali kama vile kuitumia ardhi iliyopo kuzalisha mali, yakiwemo mazao ya chakula na biashara ili kuondokana na umasikini.
Social Plugin