Mbunge wa Nzega Mjini Hussein Bashe ameonesha kutofurahishwa, baada ya yeye, Januari Makamba pamoja na Mbunge wa Mtama Nape Nnauye, kutajwa kuwa miongoni mwa watu ambao washajiunga na chama cha ACT - Wazalendo na wanasubiri kipindi cha Ubunge kiishe.
Hussein Bashe ameonesha hali hiyo kupitia ukurasa wake wa twitter baada ya mtu anayedaiwa kudukua mawasiliamo ya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe kuchapisha taarifa juu ya Wabunge hao kujiunga na ACT - Wazalendo muda wowote.
Mdukuzi ameandika kuwa "nawakaribisha pia Hussein Bashe na Nape Nnauye ambao tayari wameshachukua kadi za uanachama ACT - Wazalendo na wanachosubiri ni kuvunjwa tu kwa Bunge na bila kumsahau mdogo wangu Januari Makamba,"
Akijibu madai hayo Mbunge wa Nzega Hussein Bashe ameandika kuwa "wanaofahamu siasa za Tanzania na wanaonifahamu vizuri misimamo ama maamuzi yangu ya kisiasa, huwa sifanyi kwa njia za kificho ama za kichimvi, Siku nikiamua kuondoka CCM nitaondoka hadharani ,sitasubiri njia za kificho"
"Hili Genge la kihuni ambalo linaongozwa na wahuni wachache ipo siku nitawataja kwa majina, ila mpango wenu wakutaka kunifanya nione CCM si chama sahihi kwa mimi kuwatumikia wananchi wa Nzega na Tanzania hautafanikiwa,CCM bado nipo sana" amemaliza Bashe.