Rais Xi Jinping wa China ametangaza habari ya kutiwa saini mapatano ya kufutwa sarafu ya dola ya Marekani katika miamala ya kibiashara ya nchi yake na Russia.
Rais amesema kwamba kwa mujibu wa mapatano ya nchi mbili hizi, dola itafutwa kabisa katika mabadilishano ya kibiashara ya nchi mbili na badala yake sarafu za mataifa hayo kuchukua nafasi ya dola katika mabadilishano hayo.
Sambamba na matamshi hayo ya Xi Jinping serikali ya Russia, kupitia tovuti rasmi ya serikali ya Moscow, imetoa amri ya kuanza kutekelezwa mapatano hayo ya mabadilishano ya kibiashara kwa kutumika sarafu za nchi hiyo na China.
Kwa mujibu wa mapatano hayo ambayo yanachukuliwa kuwa waraka rasmi wa serikali za China na Russia, malipo yote ya kifedha kuhusiana na mauzo na maagizo ya bidhaa kutoka nje, huduma na uwekezaji wa moja kwa moja baina ya mashirika ya kiuchumi ya nchi mbili yatafanyika kwa kutumika ruble, sarafu ya kitaifa ya Russia na yuan, sarafu ya kitaifa ya China.
Mapatano hayo ambayo yametiwa saini katika safari ya Rais Xi Jinping mjini Moscow ni hatua muhimu ya nchi hizo katika kuimarisha thamani ya sarafi hizo mkabala wa dola ya Marekani.
Russia na China ambazo kwa sababu moja au nyingine zina mivutano ya kisiasa na kibiashara na Marekani, zimetumia njia ya kufuta dola katika miamala yao ya kibiashara na hivyo kupunguza makali ya chombo hicho muhimu ambacho kimekuwa kikitumiwa na viongozi wa Washinton kutoa mashinikizo dhidi ya nchi hizo.
Na hasa ikitiliwa maanani kwamba China hivi sasa iko katika mvutano mkubwa wa kiashara na kiuchumi na Marekani na hivyo kuwa katika mazingira ya kupata madhara makubwa kuliko Russia.
Hivyo uamuzi wa nchi mbili hizo kutumia sarafu zao za kitaifa katika mabadilishano ya kibiashara kati ya Moscow na Beijing ni hatua muhimu katika juhudi za kujaribu kupunguza mashinikizo ya Washington dhidi ya mataifa hayo.
Serikali ya Russia pia tokea wakati wa kuwekewa vikwazo na nchi za Magharibi mwaka 2014 imefanya juhudi kubwa za kuweka sarafu ya yuan ya China, ikiwa sarafu muhimu ya kigeni, katika akiba yake ya fedha za kigeni.
Kuhusiana na suala hilo, Elvira Nabiullina, Gavana wa Benki Kuu ya Russia anasema: Sera ya kufuta kabisa dola katika akiba ya fedha za kigeni na miamala ya kimataifa, ni jambo ambalo limeikinga Russia kutokana na hatari za kiuchumi na kisiasa kutoka nje.
Tunapasa kuashirika hapa kwamba mbali na uamuzi wa Russia na China kutumia sarafu zao za kitaifa katika miamala ya biashara ya pande mbili, pia zimechukua uamuzi wa kutumia sarafu ya euro katika miamala hiyo na pia kijiwekea akiba katika hazina zao za fedha za kigeni.
Katika uwanja huo Mehdad Imadi, mtaalamu wa masuala ya kiuchumi anasema: Kuchukuliwa euro kuwa sarafu ya kwanza muhimu katika akiba za benki kuu tofauti za dunia, kutapelekea kupungua kwa matumizi ya dola na hatimaye kupungua thamani yake.
Ni wazi kuwa uamuzi wa kufuta dola katika mzunguko wa kiuchumi wa kitaifa haujachukuliwa na nchi mbili za Russia na China pekee bali nchi nyingine kadhaa duniani zimechukua uamuzi kama huo na hivyo kudhoofisha kwa kiwango fulani thamani ya sarafu ya dola.
Katika miezi kadhaa iliyopita nchi za Malaysia na Uturuki zimeanzisha mikakati ya kufuta matumizi ya dola katika mifumo yao ya uchumi.
Kuhusiana na hilo, katika ripoti yake ya hivi karibuni, Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF, limesema kuwa kiwango cha dola katika akiba za fedha za kigeni za nchi tofauti duniani kilipungua sana katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka uliopita wa 2018, na nchi hizo zimekuwa zikionyesha hamu ya kuongeza sarafu za euro, yuan na pauni ya Ungereza katika akiba zao.
Kwa mujibu wa tathmini ya shirika hilo la kimataifa, kupungua huko kwa dola katika akiba za fedha za kigeni za nchi tofauti ndiko kukubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Social Plugin