Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia mtu mmoja Abdallah Bushiri Shija (42), mkazi wa Igodima Jijini Mbeya kwa tuhuma za kufanya kazi za utabibu bila kuwa na taaluma ya utabibu hususani kwa magonjwa ya wanawake wenye matatizo ya uzazi.
Mtuhumiwa baada ya kukamatwa na kuhojiwa hakuwa na kibali chochote cha kufanya shughuli hiyo wala cheti chenye taaluma hiyo na alikiri kuwatapeli wahanga hao pesa Tsh. 2,472,000 kwa madai kuwa atawasaidia.
Akizungumza na wandishi wa Habari jijini Mbeya , Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ulrich Matei amesema mtuhumiwa alikamatwa Juni 24 mwaka huu nyumbani kwake.
Kamanda Matei amebainisha kuwa baada ya kupekuliwa nyumbani kwake, Daktari huyo feki alikutwa na vifaa tiba pamoja na dawa mbalimbali ambazo zinamilikiwa na Serikali zikiwa na nembo ya Bohari ya Dawa (MSD) pamoja a nembo inayoonyesha kuwa ni mali ya Serikali.
"Baada ya kumhoji tulibaini kuwa hana taaluma yoyote ya udaktari, lakini pia yuko na baadhi ya vifaa na dawa ambazo baadhi ni za Serikali, zina nembo ya MSD na GOT, lakini pia baadhi ya wananchi walikuja kulalamika kuwa mtu huyo alishachukua fedha zao zaidi ya 2,000,000," alisema Kamanda Matei.
Amesema baadhi ya vitu alivyokutwa navyo mtuhumiwa huyo kuwa ni pamoja daftari 119 zenye taarifa za wagonjwa aliowahi kuwatibu, vipimo vya kupimia mkojo 15, dawa za kusafishia vidonda kipimo cha Malaria ambacho kinapatikana MSD pamoja na vifaa vingine.
Matei amesema kuwa baada ya taratibu kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria huku akiwataka wananchi wa Mkoa wa Mbeya kuendelea kutoa taarifa za uharifu na waharifu.
Social Plugin