Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YA TANZANIA YAPOKEA MSAADA WA MASHINE 62 ZA KUSAFISHIA DAMU KWA WAGONJWA WA FIGO


Baadhi ya mashine za kusafishia damu kwa wagonjwa wa figo zilizotolewa na kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief kwa kuongozwa na ubalozi wa Saudia Arabia nchini, zilizopokelewa leo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akimshukuru Naibu Balozi wa Saudi Arabia baada ya makabidhiano ya mashine 62 za kusafishia damu kwa wagonjwa wa figo, tukio limefanyika leo katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Afya Dkt Faustine Ndugulile akiteta jambo na Naibu Balozi wa Saudi Arabia Bw. Ahmed Bin Saleh Alghamdi wakati wa makabidhiano wa mashine 62 za kusafishia damu kwa wagonjwa wa figo zilizotolewa na kituo cha King Salman Humanitarian and Relief, tukio limefanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.
Naibu Balozi wa Saudi Arabia nchini Bw. Ahmed Bin Saleh Alghamdi akisaini mkataba wa makabidhiano wa mashine 62 za kusafishia damu kwa wagonjwa wa figo zenye thamani ya shilingi Bilion 1.55 zilizopokelewa Leo na Naibu Waziri wa Afya Dkt Faustine Ndugulile katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) wakati wa tukio la kupokea mashine 62 zakusafishia damu kwa wagonjwa wa figo, tukio limefanyika leo katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.
Na WAMJW- DSM 
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yaendelea kusogeza huduma za matibabu ya figo kwa kupokea jumla ya mashine 62 za kusafishia damu kwa wagonjwa wa figo na kuzisambaza katika Hospitali za Rufaa za mikoa nchini.

Hayo yamejiri mapema leo katika tukio la kupokea mashine hizo kutoka kwa kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief wakiongozwa na ubalozi wa Saudia Arabia nchini zenye jumla ya shilingi Bilion 1.55, lililoongozwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya jijini Dar es Salaam.

Dkt Ndugulile amesema kuwa Serikali inaendelea kusambaza na kuboresha huduma hizi na kwa sasa zinapatikana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Bugando, Hospitali ya KCMC na baadhi ya Hospitali binafsi.

"Sisi kama Serikali tumeendelea kuboresha hizi huduma, kwa sasahivi zinapatikana Muhimbili, Hospitali ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Bugando, Hospitali ya KCMC na baadhi ya Hospitali binafsi" alisema Dkt. Ndugulile 

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea kuboresha huduma hizi licha ya kuwepo changamoto ya idadi kubwa ya wahitaji wa huduma hizi huku akidai kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuna mashine 42 huku zikifanyika sesheni tatu kwa siku, na zinafanyika kwa siku 6 katika kila wiki, 

Aidha, Dkt Ndugulile amesema kuwa, msaada huo wa vifaa vitavyosambazwa katika mikoa tisa nchini ikiweko mikoa ya Tanga, Mwanza, Kigoma, Kagera, Arusha, Iringa, Mtwara, Unguja na Zanzibar, hali itayosaidia kupunguza gharama kwa kuwasogezea wagonjwa huduma hizo.

Mbali na hayo, Dkt. Ndugulile amesema kuwa ndani ya miaka mitatu Serikali imefanikiwa kupunguza magonjwa yakuambukiza kwa asilimia 50%, huku akikiri kuwa bado kuna changamoto kubwa katika kukabiliana na magonjwa yasiyo yakuambukiza kama vile kisukari, presha na figo ambayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na mitindo ya maisha.

"Timepiga hatua kubwa sana katika magonjwa yakuambukiza, ambayo tumeyapunguza kwa asilimia 50% ndani ya miaka mitatu, tumepunguza vifo na maambukizi ya Malaria, lakini tumepunguza vile vile maambukizi ya Ukimwi, sasa changamoto inayotukabili ni magonjwa yasiyo yakuambukiza kama, kisukari, presha na magonjwa ya figo"alisema Dkt Ndugulile. 

Akiongea kwa niaba ya kituo cha King Salman Humanitarian Aid and Relief Naibu Balozi wa Saudia Arabia nchini Ahmed Bin Saleh Alghamdi ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa jitihada inayoendelea kuchukua katika kutatua changamoto kwenye Sekta ya Afya na ameahidi kuendeleza ushirikiano huo baina ya nchi hizo mbili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com