Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ulipokea kifaa muhimu cha kufundishia madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa sekta ya afya, pamoja na vitabu vya kitabibu kutoka katika Jumuiya ya Watanzania waishio Uingereza wanaofanya kazi katika sekta ya afya (Tanzania United Kingdom Health Diaspora Association - TUHEDA). Makabidhiano hayo yalifanyika jijini London tarehe 22 Juni 2019.
Kifaa hicho ni sanamu ya binadamu ambayo inaendeshwa na programu maalumu za kompyuta zinazowezesha wataalamu mbalimbali wa afya kupata uhalisia wa hali ya magonjwa kama ambavyo wangeupata kutoka kwa mgonjwa aliye hai.
Sanamu hiyo iliyopewa jina la ‘Msafiri’ na Ubalozi, ina uwezo wa kupumua, kutoa sauti ya mapafu kama mtu mwenye pumu, homa ya mapafu, au mapigo ya moyo yanayoweza kuashiria shinikizo la juu au la chini la damu, sawa na mgonjwa halisi. Upatikanaji wa sanamu hiyo umefanikishwa na mwanachama wa TUHEDA, Dkt. Nasibu Mwande, mtaalamu wa masuala ya ajali na magonjwa ya dharura (Accidents and Emergency), anayefanya kazi ya udaktari hapa Uingereza.
‘Msafiri’ ana thamani ya pauni za Uingereza zisizopungua 30,000 (sawa na shilingi za Tanzania zipatazo milioni mia moja), ana umbo la kawaida la binadamu na uzito wa kilo 60. Ubalozi umetaarifiwa kuwa sanamu hiyo ni ya kwanza nchini Tanzania katika ufundishaji wa kitabibu.
Kupatikana kwa ‘Msafiri’ kutasaidia sana kupunguza makosa ya kibinadamu yanayoweza kufanywa na madaktari, wauguzi na wataalamu wengine kwani ‘Msafiri’ anaweza kutumika kutoa mafunzo ya kitabibu kwa mfano halisi wa magonjwa mbalimbali bila ya madhara ambayo yangetokea kama wataalamu wa utabibu wangetegemea kujifunza kupitia mgonjwa aliye hai.
TUHEDA pia wamekabidhi vitabu muhimu mia tatu vinavyotumika kama rejea kwa madaktari wakati wa kuamua mgonjwa apewe dawa gani, dawa zipi zinaweza kutumika kwa pamoja bila madhara, na zitolewe kwa kiwango gani. Vitabu hivyo vina thamani inayokaribia pauni 9,000 sawa na shilingi za Tanzania zipatazo milioni 30.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Social Plugin