Trump amekutana leo na Kim Jong-un, kiongozi wa Korea Kaskazini katika mpaka usiokuwa wa kijeshi wa Korea Kaskazini na Korea Kusini, ambapo Trump amevuka mstari wa mpaka huo na kukanyaga ardhi ya Korea Kaskazini.
Baada ya kuvuka mstari unaoashiria mpaka wa nchi mbili hizo jirani, Trump amesema, "Hii ni fahari kubwa kwangu, Sikutaraji. Kuuvuka mstari huu ni jambo kubwa kwangu."
Trump ameambatana na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in katika safari yake hiyo. Hii ni katika hali ambayo Trump awali alikuwa ametangaza kwamba hatokutana na Kim Jong-un katika safari yake ya Peninsula ya Korea.
Kiongozi wa Korea Kaskazini kwa upande wake amesema, "Trump amekuwa rais wa kwanza wa Marekani kuingia katika nchi yetu. Hatua hii inaashiria azma ya kufuta uhasama wa nyuma, na kufungua ukurasa mpya."
Rais wa Marekani na kiongozi wa Korea Kaskazini wamekutana mara mbili nchini Singapore na Vietnam, lakini vikao hivyo havijakuwa na tija, kwani Washington imeendelea kuiwekea Pyongyanga vikwazo, huku Pyongyanga nayo ikiendelea kufanyia majaribio makombora yake.