GGM, TACAIDS WAFANIKIWA KUANZISHA VITUO VYA KUTOA HUDUMA ZA VVU/UKIMWI


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira (wa tatu kushoto) akimsikiliza mmoja wa wajasiriamali waliowezeshwa na GGM kwa kupitia kampeni ya Kilimanjaro Chalenge, anayefuata ni Makamu wa GGM, Simon Shayo. Zaidi ya watu 65 walishuka mlima Kilimanjaro baada ya kupanda mlima huo Juni 15 mwaka huu.
Baadhi ya washiriki 65 waliopanda mlima Kilimanjaro kwa lengo la kukusanya fedha za kutokomeza VVU na Ukimwi, kampeni hiyo imeandaliwa na GGM kwa kushirikiana na Tacaids.
Makamu Rais wa GGM, Simon Shayo akizungumza katika hafla ya kuwapokea wapanda mlima 65 walioshuka Mlima Kilimanjaro Juni 22 mwaka huu baada ya kuupanda kwa siku saba kwa lengo la kukusanya fedha za kutokomeza VVU/Ukimwi.

***

Na mwandishi wetu

TUME ya Kudhibiti Ukimwi nchini kwa kushirikiana na Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) imefanikiwa kuanzisha vituo vinne vya utoaji huduma za Ukimwi na maarifa kwa lengo la kupunguza kasi ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) hasa kwa madreva wa masafa marefu.

Vituo hivyo vimeanzishwa kwa kupitia kampeni ya Kilimanjaro Challenge ambayo imelenga kukusanya fedha za kutunisha mfuko wa Ukimwi (ATF) na kutokomeza VVU na Ukimwi.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kuwapokea watu zaidi ya 80 walioshuka Mlima Kilimanjaro baada ya kupanda kwa muda wa siku saba, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Jumanne Issango alisema kampeni hiyo pia imesaidia baadhi ya vikundi vya akina mama wanaoishi na VVU kupewa mafunzo ya ujasiriamali.

Aidha, alivitaji vituo hivyo vilivyojengwa kwa kupitia kampeni hiyo ya Kilimanjaro Challenge kuwa ni Michungwani Handeni- Tanga, Manyoni Singida, Geita – Geita na Dumila- Kilosa Morogoro ambako ujenzi wake unaendelea.

Alisema vituo hivyo vitasaidia kuongeza kasi ya upimaji, upatikanaji wa matumizi sahihi ya dawa ni muhimu katika kufikia malengo ya kufikia 90 -90-90 ifikapo mwaka 2020.

“Tatizo la UKIMWI kwa Tanzania bado ni kubwa kwani kutokana na takwimu zilizopo zinaonyesha kwa kila mwaka takribanii watu 72,000 hupata maambukizi mapya ya VVU kila mwaka ambapo takriban watu milioni 1.5 wameambukizwa na VVU huku wastani wa hali ya maambukizi ikiwa ni asilimia 4.7 kwa Tanzania bara,” alisema.

Aidha, alisema wakati maambukizo hayo yakipungua kwa ujumla wake kwa watanzania yapo makundi ambayo maambukizi yamekuwa yakiongezeka hususan kwa vijana kati ya miaka 15 hadi 24.

“Makundi mengine yaliyoko kwenye mazingira hatarishi ni kama vile Wasafirishaji wa masafa marefu, watu wanaotumia dawa za kulevya, wanaofanya mapenzi kinyume na maumbile, wanawake wanaofanya biashara ya ngono, wafanyakazi kwenye migodi, wavuvi, wafanyakazi kwenye mashamba makubwa.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema jukumu lilopo ni kuwepo kwa ushiriki mpana wa wadau katika sekta zote ikiwemo sekta binafsi ndiyo maana serikali ikaanzisha Mfuko wa UKIMWI.

“Mfuko huo unalenga kuokoa kizazi chetu, kulihakikishia Taifa upatikanaji wa dawa za kufubaza VVU na kuweka mkazo ili watu wote wapime na wanaobainika kuwa wameambukizwa waanze kutumia dawa mapema na kuwa na ufuasi mzuri ili kuendelea kuishi maisha ya kawaida na kutumikia taifa,” alisema.

Aidha Makamu wa Rais wa GGM, Simoan Shayo alisema GGM itaendelea kushirikiana na TACAIDS kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ili washiriki kikamilifu kwenye afua mbalimbali za udhibiti wa UKIMWI zikiwemo za Kinga, kufanya tafiti mbalimbali, matunzo kwa wagonjwa UKIMWI, WaVIU, watoto yatima na kuweka mazigira wenzeshi.

“Ndiyo maana GGM tulianzisha programu ya Kilimanjaro Challenge Against HIV and AIDS miaka 17 iliyopita ambayo sasa imekusanya zaidi ya Sh bilioni 13 ambazo zimenufaisha taasisi mbalimbali 40 zinatoa huduma za VVU na Ukimwi pamoja na Mfuko wa Ukimwi (ATF).

"Pia imesaidia uendelezaji na uendeshaji wa Kituo cha Watoto yatima Geita (Moyo wa Huruma Orphanage Centre), Utoaji huduma za UKIMWI kwa wasafirishaji wa masafa marefu na Jamii zinazoishi kwenye maegesho hatarishi na misaada kwa kupunguza athari za UKIMWI kwa Wajane na Watoto yatima kuwapatia vifaa vya elimu,” alisema.

Timu ya wapandaji 31 wa Kili Challenge iliyoongozwa na Kapteni Moses Rusasa ilifika kileleni, 32 walitumia baiskeli waliongoza na Kapteni Masolwa Bukelebe kupitia milima na mabonde.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post