ASKOFU GWAJIMA ATINGA IKULU KUONANA NA JPM


ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Dk.Josephat Gwajima ametinga Ikulu ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza wazi kwamba ili ule Chips Mayai ni lazima baadhi ya mayai yavunjike.

Ameeleza namna ambavyo anafurahishwa na jitihada za Rais Dk.John Magufuli za kuleta maendeleo huku akitumia nafasi hiyo kumshukuru kwa jitihada zake za ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika Bonde la Mto Rufuji maarufu kwa jina la Stiegler.

Akizungumza leo Juni 3,2019 akiwa Ikulu jijini Dar es Salaam, Askofu Dk.Gwajima amesema ni jambo nzuri kutoa shukrani kwa Rais Dk.John Magufuli kwa jitihada zake za kuleta maendeleo na hasa katika kuimarisha sekta ya nishati ya umeme.

"Kwanza ni jambo nzuri kuelewa ili ule Chips Mayai lazima uvunje baadhi mayai. Kuna mayai lazima yavunje.Namshukuru Rais kwa juhudi zake katika mradi wa umeme wa Stiegler, mahala ambapo tutazalisha umeme mwingi tofauti na hapo zamani.

"Kumbuka wakati wa Mwalim Nyerere,wakati wa Mwinyi, wakati wa Mkapa na wakati wa Jakaya Kikwete tulikuwa tunazalisha umeme kiasi lakini kupitia .... tutazalisha umeme mwingi kuliko Tanzania ilipoanzia,"amesema Askofu Gwajima.

Ameongeza kama ambavyo inafahamika watu wengi wa nchi za Magharibi wanasema eneo hilo ni kwa ajili ya mazingira pamoja na mambo mengine lakini ukweli hizo ni siasa za kimataifa.

"Kwa mfano ukiangalia miaka iliyopita kulikuwa na mkataba kule Japani uliokuwa unafahamika Mkataba wa Kioto na Marekani walikataa kusaini ule mkataba.Hivyo hata sisi tunatakiwa kulinda Interest zetu,"amesema Askofu Gwajima.

Kuhusu ujumbe wake kwa Watanzania,Askofu Gwajima amesema huu ni wakati wa kukimbia na si kutembea hivyo lazima twende na kasi ya dunia."Dunia inakimbia hivyo lazima nasi Watanzania tukimbie ili twende pamoja na dunia."
Habari na Said Mwishehe,Picha na Ikulu



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Dkt. Josephat Gwajima Ikulu jijini Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post