Msemaji wa makao makuu ya jeshi la Iran, Meja Jenerali Ebulfazl Shikarchi amesema shambulizi lolote la kijeshi kutoka kwa Marekani litajibiwa vikali kwa wao kushambulia maslahi ya Marekani katika eneo hilo pamoja na kushambulia washirika wa Marekani.
Shikarchi akiongea na shirika la habari la Tesnim alitoa onyo kuhusiana na matokeo ya kuishambulia Iran kijeshi.
Shikarchi alisema hawatakuwa waanzilishi wa vita dhidi ya nchi yeyote lakini watakaposhambuliwa watajibu mapigo vikali mno.
Asubuhi ya Alhamisi iliyopita, Ofisi ya Mahusiano ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ilitangaza habari ya kusambaratishwa ndege ya ujasusi ya Kimarekani, baada ya ndege hiyo kukiuka anga na ardhi ya Iran katika eneo la Kouh-e-Mobarak katika mkoa wa Hormozgan.
Komandi ya jeshi la Marekani katika eneo la Asia Magharibi (CENTCOM) sambamba na kukiri habari hiyo ilidai kwamba ndege hiyo isiyo na rubani ya Marekani ilikuwa bado haijaingia katika anga ya Iran na kwamba ilikuwa katika maji ya kimataifa.
Social Plugin