Wanadiplomasia wa ngazi ya juu kutoka mataifa matano yaliyo na nguvu duniani wanakutana na wenzao wa Iran mjini Vienna Austria, katika juhudi za kuishawishi Tehran kutoachana na makubaliano ya pamoja ya nyukilia.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araqhchi amewaeleza waandishi wa habari mjini Vienna kuwa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa wanapaswa kuwasilisha mipango thabiti ili kupunguza athari za vikwazo vya Marekani.
Mataifa hayo ya Ulaya yanatarajia hii leo kuwasilisha mpango wa biashara baina yake na Iran unaojulikana kama Instex, ili kuepuka vikwazo vya Marekani.
Hata hivyo kuna wasiwasi kuwa mpango huo huenda usifufue mauzo ya mafuta ya Iran kwasababu makampuni na wafanyabiashara wana hofu kuwa mkataba wowote na Iran utawafanya walengwe na Marekani katika hatua zake.
Marekani ilijiondoa katika makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa mwaka 2015 na kuiweka vikwazo vipya Iran vinavyolenga sekta ya mafuta ya taifa hilo la Kiislamu.