Jeshi la Wananchi (JWTZ) limetangaza kuwachukulia hatua viongozi wa ndani na nje ya jeshi hilo na vijana waliohusika katika vitendo vya udanganyifu katika uandikishaji wa majina ya kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Udanganyifu huo ulihusisha ukiukaji wa taratibu na kughushi nyaraka na vyeti vilivyotumika katika uandikishaji huo.
Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda, akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo, alisema licha ya taratibu za uombaji kuwa wazi, baadhi ya viongozi wamebainika kutumia nafasi walizonazo kupenyeza majina ya ndugu, jamaa na rafiki ili wasajiliwe.
“Napenda kuwataarifu kuwa baada ya kubaini kuwako kwa udanganyifu huu, JWTZ/ JKT tutafanya uhakiki wa vyeti na nyaraka zote husika kwa vijana walioandikishwa tutashirikiana na ofisi ya Nida (Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa), Baraza la Taifa la Mitihani, Takukuru na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuwabaini waliofanya udanganyifu,” alisema Kanali Ilonda.
Ilonda bila kutaja uhakiki huo utafanyika lini na wakati gani, alisema utahusisha kuhakiki wa vyeti, nyaraka mbalimbali zilizokuwa zikihitajika kwenye uandikishaji huo pamoja na vyeti vya kuzaliwa na vipimo vya afya.
"Kwa kuweka usawa tutafanya uhakiki huu kwa kushirikiana na JKT, Nida, Wizara ya Elimu, taasisi zinazohusika na masuala ya rushwa, vyombo vya ulinzi na usalama, ili tuweze kuwachuja, tunataka kujiridhisha je, ni Watanzania kweli, wana afya njema, wana akili timamu, ametoka eneo husika na ana sifa stahiki, wale wenye sifa watachukuliwa, hata kama idadi yao itakuwa ndogo tofauti na matarajio yetu," alisema.
Ilonda alisema wale ambao watabainika kughushi watakamatwa na kufunguliwa mashtaka.
“Hakuna atakayesalimika labda wahame nchi, aliyeghushi vyeti na nyaraka mbalimbali kiwe cha kuzaliwa au daktari aliyetoa majibu ya uongo atakamatwa, waliowashawishi kughushi watakamatwa, waliotengeneza vyeti bandia, waliohusika kuwaandikisha vijana hao bila kuwa na vigezo, viongozi wote waliohusika kupenyeza majina wa ndani na nje ya jeshi nao watachukuliwa hatua kupitia mamlaka zao husika,” alisema.
Alisema hatua zitakazochukuliwa hazitaangalia wadhifa au cheo cha mtu kwa sababu lengo ni kusafisha nchi iwe na viongozi waadilifu na wanaofuata sheria na taratibu.
Social Plugin